Tahadhari ya Ebola yaongezeka, Tanzania ilivyojipangaTahadhari ya Ebola yaongezeka, Tanzania ilivyojipanga

Dar/mikoani. Serikali imesema imejipanga kuimarisha ulinzi wa afya mipakani kwa kushirikiana na nchi jirani na mashirika ya kimataifa, kufuatia kuongezeka kwa hofu ya kusambaa kwa Ugonjwa wa Ebola katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 18, 2026 Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema tayari wakuu wote wa mikoa iliyopo mipakani, wamepewa maelekezo ya kuhakikisha wanaimarisha ufuatiliaji wa watu wanaoingia na kutoka nchini ili kuzuia ugonjwa huo kuingia Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi Mei 16, 2026  jumla ya wagonjwa wanane waliothibitishwa maabara na wagonjwa 246 wanaoshukiwa kuwa na Ebola walikuwa wameripotiwa katika Mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku watu 80 wanaodaiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo waliripotiwa.

Wakati huohuo, Uganda imethibitisha wagonjwa wawili wa Ebola mjini Kampala jana Mei 17, 2026 mmoja wao akiwa amefariki dunia.

Wagonjwa hao walikuwa wametokea DRC, jambo lililothibitisha rasmi kusambaa kwa ugonjwa huo kuvuka mipaka ya kimataifa.

Akizungumza kuhusu tahadhari zinazochukuliwa na Serikali, Waziri Mchengerwa amesema suala la magonjwa ya milipuko si la nchi moja bali ni changamoto ya kimataifa inayohitaji ushirikiano wa pamoja.

Amesema wamejipanga kuimarisha mipakani kwa kushirikiana na nchi husika, ambazo tayari zimeathirika na ugonjwa huo.

“Wakuu wa mikoa wote walioko kwenye boda wamepewa maelekezo wanafuatilia, wanaoingia na kutoka na sisi tunashirikiana na majirani zetu kwani suala la afya si la nchi moja ni la kidunia na unapoibuka ugonjwa mnashirikiana,” amesema.

Amesema Tanzania pia inaendelea kushirikiana na taasisi za afya za kikanda kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani  (CDC) na WHO Afrika chini ya Mkurugenzi Mkuu wake, Profesa Mohamed Janabi, huku timu za wataalamu zikiwa tayari zimetumwa DRC na Uganda kufuatilia hali ya mlipuko huo.

Kauli hiyo inakuja wakati WHO ikitangaza mlipuko wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa baada ya ugonjwa huo kusambaa kutoka DRC hadi Uganda.

Kwa mujibu wa WHO, hadi sasa zaidi ya watu 246 wameripotiwa mashariki mwa DRC kuugua huku watu zaidi ya 80 wakidaiwa kufariki dunia.

Uganda nayo imethibitisha matukio mawili ya Ebola mjini Kampala, mmoja wa wagonjwa hao akifariki dunia.

Hali hiyo imeongeza tahadhari kwa nchi za Afrika Mashariki, hususan Tanzania ambayo ina mwingiliano mkubwa wa watu na biashara na nchi jirani kupitia mipaka ya ardhini, bandari na viwanja vya ndege.

Katika Mkoa wa Kagera, unaopakana na Uganda, tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Daniel Chochole amesema katika eneo la mpakani la Mtukula, ameweka mashine maalumu za kupima joto kwa wasafiri wanaotoka Uganda kuingia Tanzania.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwabaini mapema watu wanaoweza kuwa na dalili za Ebola kwa kuwa, moja ya viashiria vya awali vya ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla.

“Tumepokea maelekezo ya Serikali na tayari tumetenga Kituo cha Afya Kabyaire kitakachotumika kuhudumia wagonjwa au wahisiwa wa Ebola endapo watapatikana,” amesema.

Mbali na hilo, amesema wilaya hiyo imeandaa gari maalumu kwa ajili ya kuwabeba wagonjwa au wahisiwa kutoka maeneo mbalimbali na kuwapeleka vituo vya matibabu.

Pia, wameunda timu za ufuatiliaji wa wagonjwa vijijini pamoja na timu za elimu kwa jamii zitakazokuwa zikitoa taarifa kuhusu dalili za Ebola na umuhimu wa kuripoti mapema visa vinavyoshukiwa.

Ingawa Tanzania bado haijaripoti mgonjwa yeyote wa Ebola, wataalamu wa afya wanaonya kuwa hatari ya ugonjwa huo kuingia nchini ipo kutokana na biashara kubwa ya mipakani na usafirishaji wa bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Moja ya maeneo yanayotajwa kuwa katika hatari zaidi ni Kariakoo, kitovu kikubwa cha biashara nchini ambacho hupokea wafanyabiashara na mizigo kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki na Kati kila siku.

“Katika soko hilo maarufu, mamia ya wafanyabiashara kutoka DRC, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini huingia na kutoka mara kwa mara kwa shughuli za biashara, jambo linaloongeza umuhimu wa tahadhari za kiafya,” amesema Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Mugisha Nkoronko.

Wataalamu wa afya ya umma wamesema mazingira ya msongamano mkubwa wa watu, safari za mara kwa mara za kibiashara na mwingiliano wa karibu katika masoko yanaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko iwapo hatua za uchunguzi na elimu hazitaimarishwa.

Aidha, usafirishaji wa mizigo kupitia malori kutoka nchi jirani kwenda bandarini Dar es Salaam umeendelea kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa ukanda huu, lakini pia njia inayoweza kuongeza kasi ya usambaaji wa magonjwa ya kuambukiza endapo mifumo ya ufuatiliaji haitakuwa madhubuti.

EAC yatoa tahadhari

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) tayari imezitaka nchi wanachama kuimarisha uchunguzi katika vituo vya kuingilia nchini pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya na timu za mwitikio wa haraka.

Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa, Andrea Aguer Ariik Malueth amesema mlipuko huo unaonesha umuhimu wa nchi za ukanda huo kushirikiana kwa karibu katika kubadilishana taarifa na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji.

Kwa mujibu wa WHO, Ebola huambukizwa kupitia kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.

Dalili zake ni pamoja na homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, mwili na misuli, kutapika, kuharisha, uchovu mkubwa na wakati mwingine kutokwa damu.

Taarifa ya WHO

Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kwa sasa hakuna chanjo wala dawa maalumu zilizoidhinishwa kwa aina ya Bundibugyo, tofauti na aina nyingine ya Ebola, hali inayoongeza umuhimu wa kuchukua hatua za mapema za kudhibiti maambukizi.

Hata hivyo, shirika hilo limeonya dhidi ya kufungwa kwa mipaka, likisema hatua hizo zinaweza kuchochea matumizi ya njia zisizo rasmi ambazo ni vigumu kuzidhibiti kiafya.

Kwa Tanzania, changamoto kubwa sasa ni kuhakikisha tahadhari zinazotolewa zinafika kwa wananchi wote, hasa wale wanaofanya biashara za mipakani, madereva wa malori, wasafiri wa mara kwa mara na wafanyabiashara wa masoko makubwa kama Kariakoo.

Kadri biashara na usafiri vinavyoendelea kuunganisha mataifa ya Afrika Mashariki, ndivyo pia vinavyoongeza umuhimu wa nchi hizo kuwa na mifumo imara ya afya ya umma, uchunguzi wa mipakani na ushirikiano wa haraka wa kikanda katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa hatari kama Ebola.

Imeandaliwa na Herieth Makwetta (Dar) Bertha Ismail (Arusha) Saada Amir (Mwanza) na Alodia Dominick (Kagera)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *