Mlinzi ahukumiwa kunyongwa kwa mauaji KaratuMlinzi ahukumiwa kunyongwa kwa mauaji Karatu

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imemhukumu kunyongwa hadi kufa Jacob Ndoole (23), aliyekuwa mlinzi wa nyumba ya wageni ya Agobafra wilayani Karatu, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Oscar Patrice.

Asubuhi ya Mei 26, 2025, mwili wa Oscar ulikutwa ukiwa kwenye chumba cha walinzi katika nyumba hiyo ya wageni na pikipiki yake ikiwa pembeni.

Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 16, 2026, na Jaji Frank Mahimbali baada ya mahakama kuridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa alisababisha kifo cha marehemu kwa nia mbaya iliyopangwa.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 22274/2025, Jacob alikuwa akikabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa kuwa usiku wa kuamkia Mei 26, 2025, eneo la Manyara Kibaoni wilayani Karatu, Jacob alimuua Oscar Patrice ndani ya chumba chake cha ulinzi katika nyumba hiyo ya wageni.

Mahakama ilielezwa kuwa mwili wa marehemu ulikutwa asubuhi ukiwa ndani ya chumba cha mlinzi ukiwa na kamba shingoni huku ukiwa na michubuko usoni, shingoni na mbavuni.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mahimbali amesema ushahidi wa kitabibu uliotolewa mahakamani uliondoa uwezekano wa Oscar kujiua kama alivyodai mshtakiwa.

“Ushahidi wa kitabibu uko wazi na thabiti kwamba marehemu alikufa kwa kukosa hewa kutokana na michubuko iliyobainika, inaashiria mapambano ya kimwili na si tukio la kujiua,” alisema jaji huyo.

Ushahidi wa mashtaka

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba pamoja na vielelezo vinne, vikiwamo kamba iliyodaiwa kutumika katika tukio hilo pamoja na pikipiki ya marehemu.

Shahidi wa kwanza, Dk Michael Singay, aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alieleza kubaini michubuko shingoni, usoni na mbavuni kwenye mwili huo na kuwa chanzo cha kifo hicho ni kukosa hewa.

Shahidi wa pili, Urusulla Zakayo, alidai Mei 25, 2025, alipokuwa akirudi nyumbani alisimama karibu na nyumba hiyo ya wageni na kuona wanaume wawili, mmoja akiwa amevalia shuka la Kimasai (aliyemtambua kuwa ni mshtakiwa).

Amedai siku iliyofuata alipokwenda polisi alitambua mwili wa marehemu kuwa ni mtu aliyekuwa pamoja na mshtakiwa usiku wa tukio.

Shahidi wa tano, ambaye pia alikuwa rafiki wa marehemu na dereva bodaboda, Kelvin Patrick, alidai kumwona mshtakiwa akigombana na Oscar kabla ya kumvuta ndani ya chumba cha walinzi na kuwa alishindwa kuingilia kati ugomvi huo kwa madai kuwa mshtakiwa alikuwa na kisu mkononi ambacho alimtishia nacho, hivyo akalazimika kukimbia.

Shahidi wa sita, ambaye ni Meneja wa nyumba hiyo ya wageni, Rehema Mpanda, aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa ndiye aliyetoa taarifa ya kwanza kuhusu kifo hicho asubuhi ya Mei 26, 2025.

Alidai kuwa alipoingia katika chumba cha walinzi alishtuka kuona mwili huo na pikipiki ya marehemu ikiwa ndani ya chumba hicho na kumshauri mshtakiwa aripoti tukio hilo kwa Mkurugenzi na polisi.

Shahidi wa saba, ambaye ni Ofisa wa Polisi na mpelelezi wa kesi hiyo, alidai wakati anamhoji mshtakiwa Mei 29, 2025, mshtakiwa alidai kuwa aliingilia kati jaribio la Oscar kutaka kumbaka mwanamke mmoja na kumweka katika chumba hicho cha walinzi.

Alidai mshtakiwa alieleza kuwa Oscar alijinyonga na yeye (mshtakiwa) alikuwa akijaribu kumuokoa ndipo akakata kamba aliyokuwa anatumia kujinyonga.

Katika utetezi wake, Jacob alikana kumuua marehemu akidai kuwa alimkamata Oscar baada ya kumkuta akijaribu kumbaka mwanamke mmoja karibu na nyumba hiyo ya wageni.

Alidai kuwa baada ya kumkamata alimweka ndani ya chumba chake kabla ya marehemu kujinyonga kwa kutumia kamba.

Mshtakiwa alisema alikata kamba hiyo katika jitihada za kumuokoa kabla ya kutoa taarifa kwa meneja wa nyumba ya wageni na polisi.

Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Jaji amesema Mahakama itaangalia masuala matatu katika uamuzi wake, ambayo ni iwapo Oscar alikufa kwa kujiua, Jacob ndiye aliyehusika na kifo hicho na iwapo nia mbaya ilianzishwa chini ya kifungu cha 200 cha Kanuni ya Adhabu.

Amesema Mahakama pia ilizingatia kwamba mwili wa marehemu ulipatikana ndani ya eneo lililokuwa chini ya uangalizi wa moja kwa moja wa mshtakiwa.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mazingira yote ya tukio pamoja na ushahidi wa mashahidi yalionyesha wazi kuwa mshtakiwa alikuwa na nafasi ya kipekee ya kueleza kilichotokea kwa marehemu.

Amesema mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai na alikuwa akidhibiti chumba cha mlinzi ambacho ndani yake ndimo mwili ulipatikana.

Katika hukumu yake, Jaji Mahimbali alinukuu maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufani yaliyowahi kueleza kuwa ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kuthibitisha hatia pale unapokuwa thabiti na kuondoa uwezekano mwingine wote.

Mahakama ilisema mlolongo wa ushahidi uliotolewa uliunda maelezo yanayoonesha kuwa Oscar hakujinyonga bali aliuawa.

“Ushahidi wa upande wa mashtaka, ingawa si wa mashahidi wa macho, umeunda mlolongo thabiti unaoelekeza moja kwa moja kwenye hatia ya mshtakiwa,” amesema.

Kuhusu nia ya kuua, Mahakama ilisema aina ya majeraha aliyopata marehemu pamoja na mazingira ya tukio vilionyesha kuwepo kwa nia mbaya.

“Mahakama imeridhika kwamba upande wa mashtaka umethibitisha bila shaka yoyote kuwa mshtakiwa alisababisha kifo cha Oscar Patrice kinyume cha sheria kwa nia mbaya iliyopangwa. Mahakama inamtia hatiani kwa mauaji na inamhukumu mshtakiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa,” imehitimisha hukumu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *