
Mbeya. Wanafunzi 24 wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) wamenusurika kifo baada ya nyumba wanayoitumia kama bweni kuungua moto, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likitangaza operesheni maalumu.
Tukio hilo linaelezwa kutokea jana Mei 18 majira ya saa nane mchana katika Mtaa wa Ikuti, Kata ya Iyunga jijini Mbeya. Wakati wa tukio hilo, wanafunzi hao hawakuwepo.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema linatarajia kufanya operesheni maalumu kwa nyumba na mabweni yote yanayotumiwa na wanafunzi kuangalia ubora wake, ikiwamo mifumo ya umeme, na kutoa elimu kwa wamiliki na watumiaji.
Akizungumza leo Jumanne Mei 19, 2026, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi hilo mkoani Mbeya, Malumbo Ngata, amethibitisha tukio hilo akisema hakuna madhara kwa binadamu zaidi ya mali zilizokuwamo kwenye nyumba hiyo katika vyumba sita vilivyowaka moto.
Kamanda Ngata amefafanua kuwa nyumba hiyo iliyokuwa inatumika kama bweni ina jumla ya vyumba 24 huku sita kati ya hivyo, vikiteketea pamoja na samani zote zilizokuwa ndani.
Hata hivyo, jeshi hilo likifanikiwa kuokoa vyumba 18 na mali zake.
“Wakati wa tukio hakukuwamo mwanafunzi yeyote, hivyo hakuna vifo wala majeruhi kwa binadamu, zaidi ni vifaa kama magodoro kuungua katika vyumba sita ambavyo vimewaka moto.
“Tunashukuru tukio lilikuwa mchana na Zimamoto tulifika kwa wakati na kuokoa vyumba 18 na mali zake. Chanzo bado hakijafahamika isipokuwa tunahisi moja ya vifaa vya hita kilichokuwa kimewashwa, ila tunaendelea na uchunguzi,” amesema.
Amebainisha kuwa hilo ni tukio la pili kutokea jijini Mbeya.
Awali, lilitokea maeneo ya Forest na kwamba wanatarajia kufanya operesheni maalumu kwa nyumba na mabweni yanayotumiwa na wanafunzi.
Katika operesheni hiyo, amesema wataangalia mikataba baina ya vyuo na wamiliki wa nyumba, lengo likiwa kutoa elimu kwa watumiaji kuhusu usalama na kinga dhidi ya majanga ya moto.
“Lakini tutataka kujiridhisha na ubora wa miundombinu ya nyumba zenyewe baada ya kupata orodha yake, kujua ubora wa mifumo ya umeme na kwa sasa Mbeya yetu ina baridi,” amesema.
Kamanda Ngata amewataka wamiliki wa nyumba zinazotumiwa na wanafunzi kuhakikisha wanazingatia uimara wa miundombinu na watumiaji kuwa waangalifu wakati wa matumizi ya vifaa vya umeme.
“Watoe taarifa pia inapotokea dharura ya moto kwa mamlaka, wahakikishe miundombinu ya umeme inakuwa na tahadhari za kupambana na majanga ya moto,” amesema.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Vaileth Msombwa, amesema wakiwa katika majukumu yao ya kila siku katika eneo hilo walishtushwa na moshi mkali uliokuwa ukitoka katika nyumba hiyo, hali iliyosababisha waliite Jeshi hilo.
“Hatukujua, tulisikia tu kishindo cha moshi mzito ukifukuta kutoka kwenye nyumba hiyo na ukizingatia tunajua ni ya wanafunzi, tunashukuru Jeshi la Zimamoto lilifika haraka na huenda madhara yangekuwa makubwa,” amesema.
