Neymar ajumuishwa kikosi cha Brazil Kombe la DuniaNeymar ajumuishwa kikosi cha Brazil Kombe la Dunia

Rio de Janeiro, Brazil. Kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti amemrudisha nyota mkongwe Neymar katika kikosi cha taifa kwa ajili ya Kombe la Dunia, huku mastaa wawili wa Ligi Kuu England wakikosa nafasi hiyo.

Licha ya wasiwasi uliokuwa umetanda kuwa huenda asingeitwa, Ancelotti amemjumuisha staa huyo kikosini.

Washambuliaji Joao Pedro wa Chelsea na Richarlison wa Tottenham ni miongoni mwa waliokatwa kwenye kikosi hicho, hatua iliyoonekana kama pigo kubwa kwa nyota hao.

Ancelotti ametangaza kikosi chake usiku wa jana Jumatatu Mei 18, 2026 akiwa amewajumuisha nyota mbalimbali wa safu ya ushambuliaji akiwemo Vinicius Junior, Endrick, Raphinha, Gabriel Martinelli, Matheus Cunha, Rayan na Igor Thiago.

Hata hivyo, kilichovutia zaidi ni kurejea kwa Neymar mwenye miaka 34, ambaye sasa anakipiga Santos na anatarajiwa kucheza Kombe lake la Dunia la nne.

Kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti. Picha na Mtandao

Ancelotti amesema:

“Nilipokea ushauri mwingi sana. Kutoka kwa waandishi wa habari, waimbaji na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Sina hofu kusema kwamba tunataka kushinda Kombe la Dunia kwa sababu matarajio ni makubwa. Tutakuwa na kikosi chenye uwezo wa kucheza soka bora, chenye mshikamano na ubora.”

Amesisitiza kuwa:

“Hiki si kikosi kamili, nina uhakika na hilo. Timu itakayoshinda Kombe la Dunia haitakuwa timu kamili kwa sababu timu kamili haipo.”

Neymar ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Brazil akiwa na mabao 79 katika mechi 128, hajacheza timu ya taifa tangu alipoumia goti katika mchezo dhidi ya Uruguay Oktoba 2023.

Akizungumzia sababu za kumuacha Joao Pedro licha ya kiwango chake kizuri Ulaya, Ancelotti amesema:

“Tunajisikia vibaya kwa Joao Pedro kwa sababu kutokana na msimu aliokuwa nao Ulaya, alistahili kuwamo kwenye orodha hii.

“Kwa uelewa kamili, heshima na umahiri, tulichagua wachezaji wengine.”

Sasa macho yataelekezwa kwa Neymar kuona kama atafanikiwa kuiongoza Brazil kurejesha taji la dunia ambalo taifa hilo halijashinda tangu mwaka 2002.

Nyota wa Brazil, Neymar Jr. Picha na Mtandao

Kikosi cha Brazil

Golikipa: Alisson (Liverpool), Ederson (Fenerbahce), Weverton (Gremio)

Mabeki: Alex Sandro (Flamengo), Bremer (Juventus), Danilo (Flamengo), Douglas Santos (Zenit Saint Petersburg), Gabriel (Arsenal), Roger Ibanez (Al-Ahi), Leo Pereira (Flamengo), Marquinhos (Paris Saint-Germain), Wesley (Roma)

Viungo: Bruno Guimaraes (Newcastle), Casemiro (Manchester United), Danilo (Botafogo), Fabinho (Al-Ittihad), Lucas Paqueta (Flamengo)

Washambuliaji: Endrick (Lyon), Gabriel Martinelli (Arsenal), Igor Thiago (Brentford), Luis Henrique (Zenit Saint Petersburg), Matheus Cunha (Manchester United), Neymar (Santos), Raphinha (Barcelona), Rayan (Bournemouth), Vinicius Junior (Real Madrid)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *