
Dodoma. Serikali imetaja sababu tatu zinazosababisha kucheleweshwa kwa malipo ya kifuta jasho na machozi kwa watu walioathiriwa na wanyama wakali na waharibifu wa mazao.
Sababu hizo ni baadhi ya watu kuandika namba zenye majina yanayotofautiana, kuwa na akaunti mfu na wengine kutoandika kabisa namba zozote za utambuzi.
Kauli hiyo imetolewa Jumatatu Mei 18, 2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji wakati akijibu hoja za wabunge kutokana na hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2026/27, ambapo amesema fedha za kuwalipa wanaodai fidia zipo na wanatamani kulipa hata sasa.
Katika michango ya wabunge, wengi walilalamikia kitendo cha ucheleweshaji wa malipo hayo kiasi cha kufanya wengine kukata tamaa kutokana na ufuatiliaji kuchukua muda mrefu bila mafanikio.
Awali, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande amesema kati ya Januari hadi Mei 7, 2026 Sh9.8 bilioni zimelipwa kifuta jasho na machozi baada ya Serikali kuanzisha mfumo wa Path ambao umesaidia kufikia wadai mapema.
Chande amesema kwa sasa maagizo ni kwa kila Mkurugenzi kupeleka madai mapema kuliko kuwatuma watumishi ambao mara nyingi huishia njiani na malipo hayafiki kwa wananchi.
“Tumemwomba Rais akatuongezea Sh6 bilioni zingine na tunazo lakini watu wa kulipwa ndiyo tatizo, wengi namba zao za simu walizoandika ni tofauti na majina yao kwa hiyo fedha zikitumwa zinarudishwa,” amesema Dk Kijaji.
Waziri amesema mfumo wa sasa hakuna kuchukuliana fedha na hakuna kutumwa watumishi tena kwenda kulipa badala yake kila kitu kinakwenda kwa mfumo.
Kuhusu ongezeko la tembo, amesema sensa ya wanyama hao bado inaonyesha ni wachache ukilinganisha na idadi yao kipindi cha uhuru ambapo walikuwa 300,000 lakini kwa sasa wapo 66,000.
Hata hivyo, ametoa sababu za madhara yanayotokana na wanyama hao akisema ongezeko la watu na kusogeza huduma zao karibu na hifadhi ikiwemo kilimo ambacho kinatoa ushawishi kwa wanyama.
Ametaja njia za kuzuia madhara hayo ni kuwafunga mikanda tembo, pia wanakwenda kununua helikopta mbili kwa ajili ya kusaidia kuwafukuza kila wanaposogelea makazi ya wananchi.
Akizungumzia sekta ya utalii amekiri kuna changamoto lakini akasema wanayo mikakati ya kuhakikisha wanafanya mageuzi makubwa na akaomba wabunge wampe walau miezi sita ili kukamilisha kila kitu.
Hata hivyo, amesema wanaobeza idadi ya watalii hawaitendei mema Tanzania kwani takwimu hizo zinatolewa na Shirika la Utalii la Duniani ambazo zinafuatilia hivyo takwimu hizo ni sahihi, huku akisifia China kwa kuleta watalii wengi kuliko miaka mingine na sababu ni filamu ya Royal Tour ambayo ilikwenda kuonyeshwa kwao.
“Tanzania ni ya tatu kwa kuleta idadi ya watalii wengi na wanapofika nchini wanatumia fedha nyingi zaidi kuliko mataifa mengine duniani,” amesema Dk Kijaji.
Kuhusu uwajibikaji, amesema hadi sasa jumla ya watendaji 17 wa wizara wamesimamishwa kazi kutokana na utendaji usiridhisha ambao umepelekea manung’uniko kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi ameitisha kikao cha pamoja kwa wabunge na Serikali ili wajadili suala la kuchelewesha malipo kwa waathirika ikiwemo wanaodai fidia za mashamba katika Wilaya ya Mbarali.
Alitoa hoja hiyo kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mbarali Bahati Ndingo wakati Bunge lilipokaa kama kamati kuhusu wananchi walioondolewa katika mashamba yao, lakini miaka mitatu sasa hawajalipwa fidia.
Naye Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewaambia wabunge Serikali inakwenda kuangalia sheria ya utaifishaji akisema Rais ameshaelekeza iangaliwe upya kwani aliyebeba meno ya tembo na mkaa wote adhabu zinakuwa sawa jambo alilosema siyo sahihi.
Akihitimisha Bunge, Spika wa Bunge Mussa Zungu amesema ndani ya wizara bado kuna dhuluma zinazofanywa na baadhi ya watumishi jambo linalosababisha baadhi ya wananchi hata kuandamana.
Amesema ndani ya wizara kazi zipo lakini utu haupo akisisitiza kama ungetokea mchujo baadhi ya watumishi wa wizara hiyo wangekosa kazi hata sasa.
