Dar es Salaam. Kaka wa mwanamuziki wa bendi ya Sikinde, Abdalla Hemba, anayefahamika kwa jina la Ramadhani Hemba, amesema hali ya ndugu yake imeanza kuimarika baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini na kuendelea na matibabu nyumbani.
Akizungumza na Mwananchi, Ramadhani amesema Abdalla ameanza kula na kuongea tofauti na ilivyokuwa awali alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam akiwa katika hali mbaya kiafya.
“Hali yake sasa inaendelea vizuri tofauti na mwanzo. Ameanza kula mwenyewe na pia anaongea,” amesema Ramadhani.
Aidha, ameeleza kuwa kutolewa hospitalini kwa Abdalla hakukutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu, bali ilikuwa ni ruhusa maalum kutoka kwa madaktari waliokuwa wakimhudumia baada ya kuona mandeleo ya afya yake.
“Madaktari walimruhusu kutoka baada ya kuona ameanza kula kwa kutumia kijiko. Mwanzo alikuwa anakula kwa kutumia mipira maalum ya hospitali,” ameongeza.
Awali, familia ya Abdalla Hemba ilieleza kuwa mwanamuziki huyo alikuwa katika hali tete zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo, jambo lililowatia hofu mashabiki na wadau wa muziki wa dansi nchini.
Mwananchi pia lilimtembelea msanii huyo wakati akiwa hospitalini na kushuhudia mapambano yake ya kiafya, huku ndugu na marafiki wakimuombea apone haraka.
Mashabiki wa muziki wa dansi wameendelea kutuma salamu za pole na dua kwa Abdalla Hemba wakiamini ataendelea kuimarika na kurejea tena kwenye shughuli zake za muziki.
Abdalla Hemba alianza kuugua Machi 22, 2026 na kufikishwa Hospitali ya Malawi iliyopo Kiwalani, ambapo aligundulika kuwa na malaria pamoja na UTI, akalazwa kwa siku moja kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kutoka hospitalini hali yake ilianza kuzorota tena na kulazimika kurejeshwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Baadaye alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambako alipatiwa matibabu huku vipimo zaidi vikibaini alikuwa akisumbuliwa na maradhi malimbali ikiwemo TB, kisukari, BP, figo pamoja na mfumo wa upumuaji.
Familia yake ilieleza kuwa kwa muda mrefu walikuwa wakimpeleka hospitalini mara kwa mara kwa ajili ya kuwekewa dripu kutokana na kushindwa kula na mwili kudhoofika, lakini hali ilikuja kubadilika ghafla baada ya kupoteza uwezo wa kuzungumza na kutotambua watu waliokuwa wakimzunguka, naipo madaktari wakaamua kumlaza moja kwa moja katıka Hospitali ya Temeke chini ya uangalizi maalum.
