Tabora. Matumizi ya viuwatilifu pamoja na uchomaji moto katika misitu vimetajwa kuwa na athari kubwa kwa sekta ya nyuki nchini, ikielezwa kuwa vitendo hivyo si rafiki kwa uhai wa nyuki ambao ni nguzo muhimu katika uzalishaji wa asali.
Hayo yamebainishwa leo Mei 20, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Gerald Mongela, aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani na zoezi la kitaifa la utundikaji wa mizinga, yaliyofanyika mkoani Tabora.
Shughuli ya utundikaji wa mizinga ilifanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki kilichopo kata ya Cheyo, Manispaa ya Tabora, kisha kufuatiwa na ukaguzi wa mabanda ya maonesho ya mazao ya nyuki katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Vita, kata ya Gongoni.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua (wa tatu kutoka kulia), Gerald Mongela, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akikagua baadhi ya maeneo ya Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mkoani Tabora.
Mongela amesema baadhi ya watu wasio waadilifu wamekuwa wakichoma moto hovyo misitu, jambo linalohatarisha uhai wa nyuki na hivyo kuathiri uzalishaji wa asali bora inayotoka Tabora.
Amesema Serikali kupitia Wizara husika haitavumilia vitendo hivyo kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya nyuki katika uchumi wa nchi, hususan katika kuongeza mapato na kukuza ajira.
“Hatuwezi kukubali watu wachache waharibu juhudi za taifa kufikia lengo la kuendelea kushikilia rekodi ya uzalishaji wa asali bora Afrika,” amesema Mongela.
Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuimarisha vituo vya mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na kutangaza fursa zilizopo ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Hussein Msuya, amesema sekta ya nyuki inaendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya viwanda kupitia uchakataji wa mazao yake.
Amesema ni muhimu kuwekeza katika viwanda vya kuchakata asali na mazao mengine ya nyuki ili kuongeza thamani na kuimarisha mnyororo wa thamani.
Naye Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Daniel Panklas, amesema maadhimisho ya Siku ya Nyuki yanafanyika kwa mara ya sita, ambapo mwaka huu Tabora imepata heshima ya kuwa mwenyeji kutokana na uzalishaji wake mkubwa.
Amesema mkoa wa Tabora unachangia takribani asilimia 50 ya asali inayozalishwa nchini, akisisitiza umuhimu wa kudumisha ubora wa bidhaa hiyo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, John Mboya, amesema sekta ya nyuki pia ina mchango mkubwa katika kuwaunganisha wajasiriamali na kukuza mnyororo wa thamani kupitia bidhaa za asali na mazao yake.
Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani huadhimishwa kila Mei 20, ambapo kwa mwaka huu Tanzania itaadhimisha rasmi Mei 22 mkoani Tabora, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Uhifadhi wa nyuki kwa ustawi wa mazingira na taifa letu.”
