FIFA2026: Fahamu miamba inayopewa nafasi kwenye fainali za mwaka huuFIFA2026: Fahamu miamba inayopewa nafasi kwenye fainali za mwaka huu

Wakati zikiwa zimesalia takribani wiki tatu kwa fainali za kombe la dunia mwaka 2026 kung’oa nanga kwenye mataifa ya Marekani, Canada na Mexico, RFI Kiswahili tunazimulika timu zinazopewa nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya.

Imechapishwa:

Dakika 5 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na Hannah Nalianya

1. Timu ya taifa ya Ufaransa, inafahamika kwa jina la utani kama ‘Le Bleus’:

Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps.
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps. AFP – FRANCK FIFE

Hawa wamewahi kushinda kombe la Dunia na kupoteza fainali mbili kwa penalti katika mashindano saba ya mwisho.

Haya yatakuwa mashindano yao ya mwisho kabla ya kocha wao wa muda mrefu Didier Deschamps kuondoka.

Ufaransa waliishinda Brazil 2-1 mwezi Machi kisha wakaifunga Colambia 3-1 wakiwa na kikosi tofauti kabisa cha kuanza, mechi zote zikipigwa Marekani, ikiwa haijapoteza mechi 9 ilizocheza tangu mwezi Juni mwaka jana.

Wachezaji wanaotazamiwa kuwa chachu ya mafanikio ni pamoja na mshindi wa Ballon d’Or Ousmane Dembele, Kylian Mbappe, Michael Olise na Rayan Cherki.

2. Timu ya taifa ya Uhispania, jina maarufu la utani wanafahamika kama ‘La Roja’

Mashabiki wa soka wa Uhispania
Mashabiki wa soka wa Uhispania © Albert Gea / REUTERS

Mabingwa hawa wa Ulaya hawajapoteza mechi tangu waliposhinda Euro 2024, kikosi cha Luis de la Fuente ni kama mashine iliyokamilika, ambapo mchezaji anayeng’ara zaidi ni nyota chipukizi, Lamine Yamal, winga huyo wa Barcelona mwenye umri wa miaka 18 kwa sasa yuko nje kutokana na majeraha ya nyonga na taarifa zinaonyesha huenda akakosa mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi.

Mwenzake wa Barcelona Fermin Lopez, atakosa mashindano kabisa kutokana na kuvunjika mguu, huku mchezaji wa Arsenal, Mikel Merino, aliyefunga mabao manane katika mechi 10 kwa Hispania mwaka 2025, hajacheza tangu Januari kutokana na majeraha.

Hata hivyo “La Roja” bado wana ubora mkubwa kama Rodri (mshindi wa Ballon d’Or 2024) au Pedri.

3. Timu ya taifa ya Argentina inafahamika kwa jina la utani kama ‘La Albiceleste’

Timu ya taifa ya Argentina, wakishangilia kombe la dunia katika mashindano yaliyopita
Timu ya taifa ya Argentina, wakishangilia kombe la dunia katika mashindano yaliyopita © AFP / BEN STANSALL

Kikosi cha kocha Lionel Scaloni, kina ndoto za kutetea taji waliloshinda mwaka 2022, mashindano ambayo yalikuwa kilele cha galacha wa soka Lionel Messi, na ni vigumu kufikiria atafikia kiwango kile kile alichokuwa nacho na  mwezi ujao atafikisha miaka 39.

Hata hivyo Messi yuko nyumbani Marekani na hadi sasa amefunga mabao 12 katika mechi 13 za ligi kuu ya MLS akiwa na klabu ya Inter Miami.

Argentina pia walishinda Copa Amerika mwaka 2024 na walipita kirahisi katika mechi za kufuzu ukanda wa Amerika Kusini

Mbali na Messi, wana wachezaji wengi wa ushambuliaji kama vile Lautaro Martinez, Julian Alvarez na Nico Paz.

4. Timu ya taifa ya Uingereza, jina lake maarufu ni ‘The Three Lions’

Mshambuliaji wa klabu ya Bayern Munich na timu ya taifa ya Uingereza Harry Kane.
Mshambuliaji wa klabu ya Bayern Munich na timu ya taifa ya Uingereza Harry Kane. AFP – INA FASSBENDER

Baada ya kukaribia mafanikio mara kadhaa chini ya kocha Gareth Southgate, na kushindwa maraa kadhaa katika fainali mbili za mwisho za Euro na kuondolewa robo fainali ya kombe la dunia mwaka 2022, Uingereza sasa wanatumai Mjerumani Thomas Tuchel atawasaidia kushinda taji lao la kwanza tangu 1966.

Uingereza walipita hatua ya kufuzu kwa urahisi lakini kuna mashaka kidogo kwani walitoka sare na Uruguay na kufungwa na Japan katika mechi za kirafiki mwezi Machi.

Majina makubwa kama Jude Bellingham na Cole Palmer hawajakuwa na misimu rahisi, hata hivyo wanamtegemea Harry Kane, ambaye amefunga mabao 58 msimu huu akiwa na klabu ya Bayern Munich.

5. Timu ya taifa ya Ureno, jina maarufu la utani ni ‘A Selecao’

Mshambuliaji mkongwe wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo.
Mshambuliaji mkongwe wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo. REUTERS – Hamad I Mohammed

Ureno, ambao hawajawahi kufika zaidi ya nusu fainali, ni washindani wa kweli, mradi tu wasizuiliwe na uwepo wa Cristiano Ronaldo.

Akiwa na miaka 41, hii itakuwa fainali yake ya sita ya kombe la Dunia, hata hivyo ubora wa viungo wao kama Vitinha, Joao Neves, Bernardo Silva na Bruno Fernandes unaweza kuwa muhimu.

Wameshinda Nations League mwaka jana lakini walipata changamoto kwenye kufuzu, wakifungwa na Ireland baada ya Ronaldo kutolewa kwa kadi nyekundu

6. Timu ya taifa ya Brazil, inafahamika sana kwa jina la utani ‘Canarihna

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar Jr, ambaye amejumuishwa kwenye kikosi na kocha Carlo Ancelotti.
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar Jr, ambaye amejumuishwa kwenye kikosi na kocha Carlo Ancelotti. AFP – ANNE-CHRISTINE POUJOULAT

Maendeleo ya Brazil chini ya kocha mpya Carlo Ancelotti yatakuwa ya kuvutia kutazama, uamuzi wa kumleta kocha Muitaliano unaonyesha changamoto ya utambulisho wa soka la Brazil na ukosefu wa kikosi kipana.

Neymar, mwenye miaka 34, sasa anacheza Santos na hajacheza timu ya taifa tangu mwaka 2023 amejumuishwa kwenye kikosi, Vinícius Júnior ndiye kiongozi wa mashambulizi ya Brazil kwas asa.

Tangu washinde taji lao la tano mwaka 2002, Brazil wamefika nusu fainali mara moja tu, na walichapwa mabao 7-1 na Ujerumani mwaka 2014.

7. Timu ya taifa ya Ujerumani, jina lake maarufu la utani ni ‘Nationalelf’

Mshambuliaji wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani, Kai Havertz.
Mshambuliaji wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani, Kai Havertz. © AP Photo/Kirsty Wigglesworth

Kikosi cha Julian Nagelsmann kiko nyuma ya Uholanzi, Morocco na Ubelgiji katika viwango vya dunia, na inaonekana ni vigumu kusema Ujerumani wanaweza kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2014.

Waliondolewa hatua ya makundi 2018 na 2022, na wakatolewa robo fainali ya michuano ya kombe la Euro mwaka 2024 wakiwa wenyeji.

Hata hivyo ubora wa Joshua Kimmich, Florian Wirtz na Kai Havertz unawafanya waendelee kuchukuliwa kwa umakini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *