Kakoso ataka wabunge wachukue uamuzi mgumu barabara zijengweKakoso ataka wabunge wachukue uamuzi mgumu barabara zijengwe

Dar es Salaam. Mbunge wa Tanganyika mkoani Katavi, Selemani Kakoso amewataka wabunge kuchukua uamuzi mgumu ili kuhakikisha Wizara ya Ujenzi inapatiwa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya barabara na madaraja.

Kakoso ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, amesema kila mbunge anahitaji kuona barabara kwenye eneo lake inajengwa ama kukarabatiwa, lakini ukweli ni kuwa Wizara hiyo haipatiwi fedha za kutosheleza.

Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Jumatano, Mei 202, 2026 Kakoso amesema anafahamu atazodolewa, lakini ushauri wake wa kuwekwa kwa tozo ya Sh100 katika muda wa maongezi ya simu za mkononi kunaweza kuliwezesha Taifa kukusanya fedha za kutosha kumaliza kilio cha uharibifu na uchakavu wa miundombinu.

“Najua watu watanisema ila ndio ukweli, tunahitaji kuchukua uamuzi mgumu kwa sababu hata tukishika mshahara wa waziri haiwezi kusaidia. Serikali inatekeleza miradi mingi na Wizara ya Ujenzi haijapatiwa fedha za kutosha kutekeleza kila mradi. Ipo miradi mingi imeanza kutekelezwa lakini haijakamilika kwa sababu fedha hazitoshelezi.

“Nashauri Serikali iongeze tozo ya Sh100 ya muda wa maongezi kwenye mawasiliano ya simu ili fedha zitakazopatikana ziende kusaidia kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara hasa vijijini,” amesema Kakoso.

Itakumbukwa Aprili 13, 2026 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Kakoso alishauri kuwekwa kwa tozo hiyo ili kuchochea kasi ya miradi ya ujenzi.

Hata hivyo, alikosolewa vikali na wadau mbalimbali, ambao walieleza kuwa Serikali inaweza kubana matumizi ili kukusanya fedha za kuchochea kasi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo bila kumuongezea mwananchi mzigo.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akiwasilisha bajeti ya mwaka 2026/27 leo Jumatano, Mei 20, 2026 bungeni jijini Dodoma.

Mapema leo Jumatano, Mei 202, 2026 Kakoso amesema pendekezo hilo linaweza kuiingizia Serikali zaidi ya Sh1 trilioni ambazo zikielekezwa kwenye kupunguza changamoto ya uharibifu wa miundombinu, Tanzania itakuwa salama.

“Uwezo wa Serikali katika makusanyo hapo ndipo ulipoishia hivyo, lazima tuchukue uamuzi mgumu humu humu bungeni ili kunusuru miundombinu iliyoharibika vibaya na mvua. Wizara nendeni mkakamilishe barabara mlizoanzisha, pili hakikisheni barabara zinajengwa kwa mfumo wa PPP, mfano ile barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro tafuteni wabia hawawezi kuacha kuwekeza barabara inayotumia malori zaidi ya 10,000, lazima wawekeze,” amesema.

“Kwenye tozo ya Sh100 ya maongezi itumike kuchangia huduma za barabara vijijini. Sh1.1 trilioni tutakazopata Sh600 bilioni tuwape Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Sh500 bilioni tuwape Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mtashuhudia maendeleo nchi nzima,” amesema Kakoso.

Hata hivyo, katika kuhakikisha miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja haikwami, Serikali imetangaza mkakati wa kutafuta fedha katika soko la mitaji na dhamana kupitia mfumo wa hati fungani ili kuongeza uwezo wa kugharamia matengenezo ya barabara za kimkakati nchini.

Awali, akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2, Ulega mesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kunakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo maalum ya barabara muhimu zinazobeba shughuli za uchumi, biashara na usafirishaji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Amesema sambamba na mpango huo, Bodi ya Barabara itaendelea kugharamia maboresho ya Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimali za Barabara (RAMs) inayotumika kusimamia mtandao wa barabara za kitaifa na wilaya ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa matengenezo ya miundombinu hiyo.

Timothy apongeza miradi mikubwa Dar

Kwa upande wake, Mbunge wa Kawe, Geofrey Timothy ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu jijini Dar es Salaam, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza tatizo sugu la foleni linalochangiwa na ongezeko la watu na magari.

Timothy amesema uamuzi wa Serikali kukubali ujenzi wa madaraja ya juu (flyover) katika maeneo ya Mwenge na Morocco ni hatua kubwa itakayosaidia kuongeza mtiririko wa magari na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.

Amesema pamoja na miradi hiyo, bado kuna umuhimu wa kuendelea kujenga flyover nyingine katika makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kinondoni pamoja na eneo la Rainbow ili kuendana na kasi ya ukuaji wa jiji la Dar es Salaam.

Mbunge huyo pia amepongeza Serikali kwa kuridhia upanuzi wa Barabara ya Mwai Kibaki na Tegeta hadi Bagamoyo, akieleza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa uchumi wa jiji na maisha ya kila siku ya wananchi.

Aidha, ameutaja umuhimu wa kupanuliwa kwa Barabara ya Kilima cha Wazo kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa ajali nyingi eneo hilo, huku akisisitiza hatua za haraka zichukuliwe kuokoa maisha ya wananchi.

Nape atangaza kushika shilingi

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtama Nape Nnauye ametishia kushika shilingi akisema hataunga mkono wala kupitisha bajeti hiyo kwa kile alichoeleza kwamba, haijatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi-Mtwara.

Amesema barabara hiyo ni kiungo cha mikoa kadhaa ya Kusini na iliahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba itajengwa lakini anashangaa haijatengewa fedha kwenye bajeti hiyo.

Amesema wananchi wa jimbo lake wamemtuma asipoona fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, aipinge isipitishwe.

“Barabara zetu zinaharibika Serikali tumeamua kupuuza sheria hii iliyotungwa na Bunge. Hii miradi itakufa tu. Serikali kama inataka tubadilishe sheria ili muendelee kubaki na hela. Siungi mkono bajeti hii na nikiunga mkono itakuwa ni usaliti kwa wananchi wa Mtama,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *