
Dar es Salaam. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, ametishia kushika shilingi akipinga kupitishwa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, kwa madai kuwa haijatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi-Mtwara.
Nape, amesema barabara hiyo ni kiungo cha mikoa kadhaa ya kusini na iliahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba itajengwa lakini anashangaa haijatengewa fedha kwenye bajeti hiyo.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatano Mei 20, 2026 wakati akichangia mjadala wa bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2026/27 ya Wizara ya Ujenzi iliyowasilishwa na waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, Abdallah Ulega.
Amesema wananchi wa jimbo lake wamemtuma asipoona fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, aipinge isipitishwe.
Nape, amesema ameangalia randama na kuipitia mara nne, hakuona fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo tayari muda wa matumizi yake umekwisha.
“Wamezibaziba mpaka haiwezekani kuzibaziba tena. Barabara hii haikutengewa fedha, mimi nikiunga mkono bajeti hii nitawasaliti wananchi wa kusini, nitakuwa nasaliti wa ilani ya uchaguzi ya chama changu (CCM).”
“Kwa hiyo natangaza wazi kabisa, siungi mkono bajeti hii mpaka fedha itengwe kwenye hii barabara,” amesema.
Mbunge huyo, ameeleza Serikali ikitaka akubali kupitisha bajeti hiyo, itengwe fedha kwa ajili ya utekelezaji wa angalau kilomita tano za ujenzi wake.
Nape, amesema haiwezekani kuruhusu bajeti hiyo, wakati hata Rais Samia aliahidi kuijenga, akisisitiza wabunge wa kusini watasimama naye kwenye hilo kushinikiza fedha itengwe.
“Fedha itengwe kwenye hii barabara ili tuelewane, vinginevyo kutupeleka kwenye hati fungani ni changa la macho. Tengeni fedha tutawaeleweni msipotenga fedha, kwa unyenyekevu sana siwezi kuwasaliti wananchi wangu wa kusini,” amesema.
Jambo lingine alilolisimamia kidete ni kutozingatiwa kwa Sheria Namba 220 iliyoanzisha Mfuko wa Barabara unaohusisha kuhifadhi fedha zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya miundombinu hiyo.
Katika maelezo yake, amesema ukiacha kiwango kidogo cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya mfuko huo, hakitumiki kwa ujenzi wa barabara kinapelekwa kwenye miradi mingine.
“Barabara zetu zinaharibika kwa sababu Serikali tumeamua kupuuza sheria iliyotungwa na Bunge ya kutunza fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
“Maneno haya Mwenyekiti amesema, CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) anasema hatufanyi chochote, jamani tunataka kwenda wapi, barabara zitakufa Ulega tutakamata kichwa chako bure,” amesema.
Ametaka fedha hizo zipelekwe kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara badala ya kupelekwa kwingineko.
