
Serikali ya Uganda inasema zaidi ya watu 100 wamewekwa karantini huku maafisa wa afya wakijitahidi kudhibiti mlipuko nadra wa Ebola unaohusishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo.
Watu hao wamewekwa katika eneo lisilojulikana huku timu za matibabu zikichunguza dalili za maambukizi ya Ebola. Maafisa wanasisitiza kwamba hali bado inadhibitiwa na kwamba uzoefu wa Uganda katika kushughulikia milipuko ya awali umeimarisha uwezo wake wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Alan Kasujja, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Vyombo vya Habari cha Uganda na Mratibu wa Mawasiliano wa Kikosi Kazi cha Ebola, amesema nchi hiyo inategemea wafanyakazi wa afya wenye uzoefu kudhibiti hali hiyo.
“Unachohitaji kujua kwa sasa ni kwamba zaidi ya watu 100 wametambuliwa na wanawekwa karantini, na wanatibiwa na wataalamu wa afya wenye uzoefu mkubwa,” Kasujja amesema na kuongeza kuwa, Uganda hapo awali iliweza kudhibiti milipuko ya Ebola, COVID-19, na VVU/UKIMWI kwa ufanisi. Ausihi umma kuendelea kuwa na uangalifu na kufuata miongozo ya afya.
Haya yanajiri huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likionya kuhusu “kiwango na kasi” ya mlipuko mbaya wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Maafisa wa Kongo wanasema kwa uchache watu 131 wamefariki dunia na zaidi ya visa 500 vinavyoshukiwa vimeripotiwa, na kuzua hofu kwamba virusi hivyo vinaweza kuenea zaidi katika kanda mzima.
