Tanzania yatumia urithi wa utamaduni kujitangaza kimataifaTanzania yatumia urithi wa utamaduni kujitangaza kimataifa

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Said Yakubu amesema nchi inaendelea kutumia vyakula vya asili na urithi wa diplomasia ya utamaduni kama nyenzo ya kujitangaza kimataifa.

Balozi Yakubu amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Afrika inayofanyika katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco)  jijini Paris, Ufaransa.

Amesema ushiriki wa Tanzania katika maonyesho hayo umeendelea kufungua fursa za kuitangaza nchi kupitia sekta ya utalii, urithi wa utamaduni na vyakula vya asili.

Kwa mujibu wa balozi huyo, Tanzania imetumia jukwaa hilo kuonesha utajiri wa mila na desturi zake pamoja na vivutio vya kipekee vya utalii vilivyopo nchini.

Ameeleza kuwa mwitikio wa wageni waliotembelea banda la Tanzania ulikuwa mkubwa, huku wengi wakivutiwa na maonyesho ya mifumo ya jadi ya uchotaji na uhifadhi wa maji pamoja na urithi wa utamaduni wa Tanzania.

Aidha, vyakula vya Kitanzania vilikuwa sehemu ya kivutio kikubwa katika banda hilo, ambapo wageni walipata nafasi ya kuonja pilau, mishikaki, mihogo na kachumbari.

Katika hafla hiyo, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Francophonie wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Thérèse Kayikwamba-Wagner, ambaye alitembelea banda la Tanzania.

Hafla hiyo imewakutanisha mawaziri kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, viongozi wa Unesco, mabalozi pamoja na diaspora wa Afrika wanaoishi Ufaransa.

Wiki ya Afrika katika Unesco hutumika kama jukwaa la mataifa ya Afrika kuonyesha mchango wa bara hilo katika utamaduni, elimu, sayansi na maendeleo ya jamii duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *