Beşiktaş , Uturuki. Aston Villa imeandika historia mpya Ulaya baada ya kuibuka mabingwa wa Europa League kwa kuichapa Freiburg mabao 3-0 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tüpraş jijini Beşiktaş huko Uturuki.
Mashabiki wa Villa waliokuwa wakisimuliwa hadithi za ubingwa wa Ulaya wa mwaka 1982 mjini Rotterdam, sasa wamepata usiku wao mpya wa kukumbukwa.
Villa ilianza kufanya mashambulizi mapema, lakini ililazimika kusubiri hadi dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kupata bao la kwanza.
Dakika ya 42, Youri Tielemans aliifungia Villa bao la kwanza kwa shuti kali baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Morgan Rogers.
Bao hilo lilionekana kuipa Villa nguvu mpya na dakika chache baadaye Buendia akaongeza la pili kwa shuti kali kutoka umbali wa mita 20.
Villa ilirejea kipindi cha pili ikiwa na kasi ileile na dakika chache baadaye Morgan Rogers akafunga bao la tatu baada ya kutumia pasi kutoka kwa Buendia.
Baada ya mchezo kumalizika mshambuliaji Ollie Watkins amesema utulivu wa kocha wao ulikuwa tofauti na inavyokuwa.
Wachezaji wa Aston Villa wakati wakishangilia ubingwa wa Kombe la Europa League baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Freiburg, Mei 20, 2026. Picha na Mtandao
“Leo alikuwa mtulivu sana wakati wa maandalizi. Wakati mwingine kwenye mechi za ligi huwa na msisimko mkubwa kwa sababu anataka ushindi, lakini leo alikuwa mtulivu na hilo liliweka mazingira mazuri kwetu.”
Aliongeza:
“Wakati mwingine unapitia vipindi vya juu na chini, lakini tuliendelea kupambana hadi mwisho. Tumefuzu Ligi ya Mabingwa tena na huu ni usiku maalumu sana.”
Kwa ushindi huo, Emery ametwaa taji lake la tano la Europa League, akiendelea kuthibitisha ubora wake katika michuano hiyo ya Ulaya.
