Manchester, England. Kiungo wa Manchester United, Casemiro amekaribia kujiunga na Inter Miami baada ya kuripotiwa kufikia makubaliano binafsi na klabu hiyo ya Marekani huku akitarajiwa kuondoka old trafford baada ya Ligi Kuu England kumalizika.
Nyota huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 34, ameripotiwa kuvutiwa na maisha ya Miami pamoja na familia yake, huku upande wa soka akivutiwa zaidi kucheza sambamba na Lionel Messi.
Inaelezwa kuwa Casemiro amekuwa akifanyia kazi kushusha mshahara wake ili kuendana na bajeti ya Inter Miami pamoja na sheria za Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Kiungo wa Manchester United, Casemiro wakati alipokuwa akipiga picha na Kombe la FA msimu wa 2023/2024. Picha na Mtandao
Inter Miami kwa sasa haina nafasi ya wazi kusajiri mchezaji maalumu, jambo linalomaanisha mkataba wa Casemiro unaweza kuwa wa dola milioni 1.8 kwa msimu wa kwanza, isipokuwa nyota mmoja wa timu hiyo akiondoka.
Januari mwaka huu Casemiro alitangaza kuwa angeondoka Manchester United mwishoni mwa msimu huu.
Licha ya kutarajiwa kuondoka, kiungo huyo alikuwa na msimu mzuri katika kipindi cha mwisho chini ya kocha Michael Carrick, kiasi cha baadhi ya mashabiki wa United kutaka aongeze mwaka mmoja zaidi klabuni hapo.
Wakati Casemiro akielekea kuondoka, Manchester United pia inaendelea na mipango ya kusuka kikosi upya, huku ikipanga kuongeza viungo wasiopungua wawili kutokana na Manuel Ugarte kutarajiwa kuondoka pia.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuwindwa na United ni Ederson wa Atalanta na Mateus Fernandes wa West Ham.
Kiungo wa zamani wa Real Madrid ambaye kwa sasa anakipiga Manchester United, Casemiro. Picha na Mtandao
Casemiro ambaye alikulia katika akademi ya kukuzia vipaji ya São Paulo huku Brazil, alijiunga na Real Madrid mwaka 2013 na alifanikiwa kushinda mataji matao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na mataji matatu ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.
Akiwa na Manchester United, kiungo huyu Mbrazil amefanikiwa kushinda mataji mawili ya Kombe la Carabao msimu wa 2022/2023 pamoja na Kombe la FA msimu wa 2023/2024.
