ZIFF 2026 yapokea filamu 400, 65 zapenya hatua ya mwishoZIFF 2026 yapokea filamu 400, 65 zapenya hatua ya mwisho

Zanzibar. Filamu 65 zitachuana kuwania tuzo katika Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu (ZIFF) linalotarajiwa kuanza kufanyika Juni 24 hadi 28, 2026 visiwani Zanzibar.

Filamu hizo zilizochaguliwa ni kati ya filamu 400 zilizowasilishwa kushiriki katika tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka.

Akizungumza Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Hatibu Madudu amesema kwa mwaka huu wamepokea jumla ya filamu 400 idadi ambayo ni tofauti na mwaka jana ambapo walipokea zaidi ya filamu 430.

“Mwaka huu tumepokea zaidi ya filamu 400 zilizotengenezwa mwaka 2025 na 2026 kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku Afrika Mashariki ikichangia takribani filamu 129.

Uganda imetuma filamu 50, Tanzania 45, Kenya 23, Rwanda 3, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 1 na Somalia filamu 7.

“Nchi nyingine zilizowasilisha idadi kubwa ya filamu ni pamoja na Afrika Kusini, Iran, Marekani na Nigeria. Pia tumepokea mawasilisho kutoka India, Brazil, China, Korea Kusini, Ufaransa, Italia, Uturuki, Argentina, Hispania, Poland, Uingereza, Ujerumani, Canada, Indonesia, Urusi, Qatar, Japan, Falme za Kiarabu, Pakistan, Tunisia, Angola, Malawi, Portugal, Ubelgiji, Luxembourg, Trinidad na Tobago, Mauritius, Msumbiji, Uzbekistan, Cameroon, Sweden, Colombia, Panama, Misri, Ukraine, Denmark, Finland pamoja na Ethiopia.” Amesema Madudu. 

Aidha Madudu amesema 
filamu zilizochaguliwa zinajumuisha filamu 14 ndefu, filamu 13 za makala, tamthilia 10 za televisheni, filamu fupi 22 na filamu 6 za animesheni, ambapo jumla ya filamu ni 65.

“Tunawashukuru sana wachambuzi wa awali kwa moyo wao wa kujitolea na msaada mkubwa walioutoa katika mchakato wa uchaguzi, makundi ya ushindani ya ZIFF mwaka huu ni Filamu Bora Ndefu, Filamu Bora Makala, Tuzo ya Emerson kwa Filamu Bora ya Zanzibar, Filamu Bora Fupi, Filamu Bora ya Animesheni, Filamu Bora Afrika Mashariki, Muigizaji Bora wa Kiume Afrika Mashariki, Mwigizaji Bora wa Kike Afrika Mashariki, Muigizaji Bora wa Kiume Tanzania, Mwigizaji Bora wa Kike Tanzania, Tuzo ya Mwenyekiti wa ZIFF pamoja na Tuzo ya Chaguo la Watazamaji kwa tamthilia za televisheni kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.”amesema Madudu 

Aliongeza kuwa;
“Mwaka huu tutaonesha filamu maalum “We Are Hadza” iliyoandaliwa na jamii ya Wahadza pamoja na wadau wao. Filamu hiyo ni ya makala iliyoongozwa na Hannah Sparkman.”

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZIFF Joseph Mwale, amesema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Akili unde (AI) na sanaa ya usimuliaji wa hadithi,” kwamba ni dhana inayogusa kwa kina muktadha wa Afrika. Pia kaulimbiu hii inaalika kuchunguza mwingiliano kati ya akili unde na changamoto za kipekee zinazoikabili Afrika katika kutumia uwezo wa AI kwa ajili ya usimuliaji wa hadithi.

“Ingawa AI inatoa njia bunifu za usimuliaji wa hadithi kama vile kuboresha utengenezaji wa maudhui na kuwezesha uzoefu wa kina zaidi, Afrika bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji kushughulikiwa.

Changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa miundombinu, ambapo huduma duni za intaneti na umeme zinazuia matumizi ya teknolojia.

“Upungufu wa data za ndani pia unapunguza uhalisia wa simulizi zinazotengenezwa kwa kutumia AI, hivyo kuwepo haja ya kukusanya na kuhifadhi hadithi zenye uhalisia wa kitamaduni.

Aidha, pengo kubwa la ujuzi katika sekta ya AI linapunguza idadi ya wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia hii kwa usimuliaji wa hadithi.

“Mazingira ya kisheria na sera pia yanapaswa kubadilika ili kusaidia matumizi ya AI yenye maadili, kuhakikisha sauti mbalimbali za Waafrika zinaimarishwa badala ya kupuuzwa.

Tunapohudhurisha urithi wetu mkubwa wa kitamaduni kupitia usimuliaji wa hadithi, ni muhimu kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hizi. ZIFF 2026 inatoa jukwaa la kuchunguza namna AI inaweza kuboresha simulizi zetu huku ikihamasisha ubunifu, ushirikishwaji na maadili, na hatimaye kuunda mustakabali ambao hadithi za Afrika zitagusa dunia nzima.”amesema Mwale.

Aliongeza “tumeandaa mafunzo maalum yanayohusu elimu ya fedha, matumizi ya AI katika utengenezaji wa filamu, uundaji wa maudhui ya kidijitali pamoja na mbinu za usambazaji wa maudhui.
Lisa Russell, mshindi wa tuzo ya Regional Emmy na Balozi wa Women in AI nchini Kenya, ataongoza warsha mbalimbali.

“Robert Mwampembwa atatoa mada kuhusu akili unde na nguvu ya uundaji wa maudhui (Esports), huku Female Film Makers in Kenya (FEFKA) wakitoa mada kuhusu elimu ya fedha kwa watengenezaji filamu wanawake.
Mzee John Kitime ataendesha kipindi maalum kuhusu uwekaji wa video za muziki katika mfumo wa kidijitali.

“ZIFF inaungwa mkono na jamii kupitia maonesho ya wazi katika Stone Town, vitongoji na vijiji. Kupitia programu hii, wananchi wa Zanzibar hupata fursa ya kufungua mijadala ya kitamaduni na tamaduni nyingine kupitia filamu katika maeneo ya umma.

Tamasha hili hufikia watazamaji zaidi ya 200,000 katika ukanda huu na kuchangia uelewa bora wa sinema.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *