JAB yasisitiza maofisa habari nao kujisajiliJAB yasisitiza maofisa habari nao kujisajili

Morogoro. Maofisa habari wa taasisi za Serikali na binafsi nchini wametakiwa kutojitenga na mfumo wa usajili wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa kigezo cha kuwa watumishi wa taasisi hizo, ikielezwa kuwa nao ni sehemu ya taaluma ya habari na wanapaswa kutambulika kisheria kupitia bodi hiyo.

Hatua hiyo imekuja huku ikielezwa kuwa baadhi ya maofisa habari waliopo kwenye taasisi mbalimbali wametokea katika taaluma tofauti, hali inayolifanya suala la usajili na uthibitisho wa kitaaluma kuwa muhimu katika kudhibiti usambazaji wa habari zisizo sahihi na kuimarisha weledi katika sekta ya habari.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari Morogoro, leo Mei 21, 2026 Ofisa Habari Mkuu wa JAB, Prudence Constantine amesema waandishi wa habari pamoja na maofisa habari wanaotakiwa kusajiliwa ni wale wenye sifa zinazotambulika kisheria ikiwemo vyeti vya diploma na shahada za taaluma ya habari.

Constantine amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha waandishi wenye taaluma wanaingia kwenye mfumo rasmi wa ithibati.

“Serikali imedhamiria kuwaingiza wale wote wanaojihusisha na habari kuanzia wapiga picha, waandishi, wahariri na maofisa habari wa taasisi za Serikali na binafsi katika mfumo kusajiliwa bodi ya ithibati ili kuwatambua kama waandishi wenye vigezo, wanaotambulika,” amesema Constantine.

Amesema suala hilo si la mzaha kwani mfumo utaendelea kuwaondoa ambao hawatazingatia matakwa ya usajili wa bodi hiyo.

Aidha, amesema wale ambao bado hawajakidhi vigezo vya kitaaluma wanapaswa kurejea vyuoni ili kukamilisha elimu inayotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Katibu wa waandishi wa habari Morogoro, Lilian Kasenene amesema kuanzishwa kwa JAB kumesaidia kuongeza idadi ya wanachama wa klabu hiyo kutokana na umuhimu wa waandishi kuwa na ithibati.

Kasenene amesema kwa sasa mwandishi anayetaka kujiunga na klabu hiyo analazimika kuwa na kitambulisho cha JAB kinachomtambua rasmi kama mwandishi wa habari.

Naye, Mratibu wa chama hicho Morogoro, Thadei Hafigwa amesema uwepo wa mfumo wa JAB, umefungua ukurasa mpya katika tasnia ya habari kwa kuongeza mnyororo wa thamani katika utengezaji wa maudhui.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *