
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma imekataa maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ya kuamuru apelekwe Dodoma kwa ajili ya kusikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mawakili wake wakipinga kuzuiwa kuonana naye kwa faragha.
Lissu alikuwa ameomba kesi hiyo isikilizwe kwa mdomo badala ya maandishi kama ilivyopendekezwa na mahakama, huku akiomba apelekwe Dodoma kusikilizwa ana kwa ana.
Katika uamuzi uliotolewa leo Alhamisi Mei 21, 2026 na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Amir Mruma, Angelo Rumisha na Everist Longopa, mahakama imeelekeza shauri hilo liendelee kwa njia ya maandishi.
Mahakama imesema sheria inaruhusu usikilizwaji kwa mdomo au maandishi na kwa kuzingatia mazingira na muda, njia ya maandishi inafaa zaidi. Hata hivyo, ilielekeza Lissu apewe huduma muhimu zitakazomwezesha kufanya utafiti na kuandaa hoja zake pamoja na haki ya kuonana na wakili wake.
Katika hatua nyingine, Mahakama imekubali ombi la Lissu la kuwaita na kuwahoji watu waliokula viapo kinzani kwa upande wa wadaiwa, hususan upande wa Magereza.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 7300/2026 imefunguliwa na mawakili Kulwa Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Mkuu wa Magereza, Mkuu wa Gereza la Ukonga na Lissu mwenyewe.
Mawakili hao wanapinga vikwazo wanavyodai kuwekwa wanapokwenda kuzungumza na mteja wao gerezani, wakisema wananyimwa faragha au kuzuiwa kupeleka nyaraka muhimu zinazohusiana na kesi zinazomkabili.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola alipinga maombi ya Lissu akidai kuwa haki ya kusikilizwa inaweza kutekelezwa hata kwa maandishi na kupelekwa Dodoma kunaweza kuathiri mwenendo wa kesi nyingine zinazomkabili Dar es Salaam.
Lissu aliieleza Mahakama kuwa akiwa mahabusu hana fursa ya kutumia maktaba, mtandao wala kupata huduma kamili za mawakili wake jambo linalofanya iwe vigumu kwake kujiandaa kwa usikilizwaji wa maandishi.
“Mimi ndiye najua viatu ninavyovivaa na ugumu wa kujitetea katika mazingira niliyomo. Sina maktaba, sina intanmeti na mawakili wangu wanazuiwa kufanya kazi yao,” alisema Lissu.
Mawakili wa Lissu, John Seka na Ferdinand Makore waliunga mkono maombi hayo wakidai haki ya kusikilizwa kwa usawa inapaswa kuzingatiwa.
Katika shauri hilo, wadai wanaitaka mahakama itamke kuwa hatua ya maofisa magereza kusikiliza mazungumzo yao na Lissu ni kinyume cha sheria, kanuni za magereza na Katiba, huku wakitaka wapewe haki ya kuzungumza na mteja wao kwa faragha.
