Mtandao wa siri wa utoaji mimba Dar huu hapaMtandao wa siri wa utoaji mimba Dar huu hapa

Dar es Salaam. Ndani ya mitaa yenye pilika nyingi ya Jiji la Dar es Salaam, nyuma ya mageti ya bati na nyumba za kupanga zisizohoji wageni wanaoingia na kutoka, kuna mtandao wa siri unaofanya kazi kimya kimya.

Hauna bango, leseni wala usajili rasmi. Lakini kwa wasichana na wanawake wengi wanaokabiliwa na ujauzito usiotarajiwa wanaufahamu, huduma zake hupatikana kwa urahisi moja kwa moja au kwa mawasiliano ya simu au ujumbe wa WhatsApp.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini uwepo wa mtandao wa watu wanaojiita wauguzi wa kujitegemea, wauzaji wa dawa kwa siri, watoa huduma wasio na vibali pamoja na madalali wanaoratibu utoaji mimba usio salama nje ya mfumo rasmi wa afya.

Imebainika kuwa mtandao huo unaendelea kustawi kutokana na hofu, unyanyapaa wa kijamii, sintofahamu ya kisheria na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi.

Hili linafanyika kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Penal Code) Sura ya 16. Kifungu cha 150, 151, 152 na 219 ambavyo vinapiga marufuku utoaji mimba kwa namna isiyo ya kitabibu yenye lengo la kumlinda mama.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa huduma jumuishi za matunzo baada ya utoaji au kuharibika kwa mimba wa Tanzania, Serikali inatambua kuwa utoaji mimba usio salama bado unafanyika kwa siri na mara nyingi hufanywa na watu wasio na utaalamu, hali inayoweka maisha ya wanawake hatarini.

Mwongozo huo unaonya kuwa matumizi holela ya dawa kama ‘misoprostol’ kwa utoaji mimba bila usimamizi wa kitaalamu yanaweza kusababisha kutokwa damu nyingi, maambukizi, uharibifu wa kizazi na hata kifo.

Pia unasema unyanyapaa wa kijamii, hofu ya sheria na ukosefu wa taarifa sahihi ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma wanawake wengi kutafuta huduma hizo kupitia mitandao isiyo rasmi.

Alipoulizwa kuhusu Wizara ya Afya inachukua hatua gani dhidi ya vituo visivyo rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmad Makuwani anasema:

“Mwongozo wa utoaji huduma baada ya mimba kuharibika unaelekeza kwamba, utoaji wa mimba kwa sababu ambazo sio za kimatibabu ni makosa kisheria. Mwongozo huu una Legal Framework (mfumo wa kisheria) inayoelezea adhabu na makosa ya kutoa mimba,” anasema na kuongeza:

“Kwaa sasa wizara haijapata kesi ambazo ni za kutoa mimba kupitia nyumba za kupanga au mitandao ya kijamii. Kama ikitokea mwongozo utafuatwa na litachukuliwa kama kosa kisheria.”

Katikati ya sheria zilizopo, katika vyumba vya kupanga, nyuma ya kaunta za maduka ya dawa na kupitia ujumbe wa siri mtandaoni, huduma hizo zinaendelea kutolewa bila usimamizi rasmi.

Kwa baadhi ya wanawake, matukio hayo huishia kwenye maumivu ya muda na hofu ya kudumu. Kwa wengine, hugeuka safari ya karibu kupoteza maisha na kwa wengi zaidi, simulizi zao hubaki gizani.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa bila kushughulikia changamoto za huduma za afya ya uzazi, elimu, unyanyapaa wa kijamii na uelewa wa sheria, wanawake wengi wataendelea kuweka maisha yao hatarini kutoa mimba kupitia mtandao huo wa siri au njia nyinginezo.

Utafiti uliofanyika nchini mwaka 2018 ulionyesha mimba takribani milioni 2.9 hutungwa kila mwaka. Miongoni mwa hizo, milioni 1.3 hazikupangwa, mimba 430,000 hutoka au kutolewa na vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama ni asilimia 19. 

Safari huanzia mtandaoni

Akiwa amejifanya ndugu wa msichana mwenye ujauzito wa wiki sita anayehitaji msaada, mwandishi wa habari hizi aliwasiliana na baadhi ya watu waliopatikana kupitia majadiliano ya siri mtandaoni.

Dakika chache baada ya kutuma ujumbe wa WhatsApp, alipatiwa namba ya nesi ambaye alimsihi asiogope ni kitendo cha dakika mbili na kuwa amesaidia watu wengi kila siku. Alipomhoji nesi alidai kuwahi kufanya kazi katika hospitali moja ya Serikali jijini, ingawa hakutoa uthibitisho.

Alitaja gharama ya Sh150, 000 kwa ujauzito wa awali, akisema fedha hizo zinajumuisha dawa na usafishaji kizazi endapo kutatokea tatizo.

Hata hivyo, alimjulisha kuwa ikiwa ujauzito utazidi mwezi mmoja itabidi asafishwe na gharama yake inaanzia Sh250,000.

Katika mawasiliano yaliyofanyika kwa siku kadhaa, watu wengine wasiopungua sita walitoa huduma zinazofanana za siri, za haraka na zinazolipwa kwa fedha taslimu.

Baadhi yao walitaka kukutana na mtaka huduma (mwandishi) maeneo ya Buguruni, Sinza na Kinondoni Mkwajuni huku wengine wakiahidi kufika nyumbani kwa mhusika wakiwa na dawa na vifaa.

Hakuna aliyedai kuona rekodi za afya kabla ya kutoa huduma (ikiwemo uhakika wa vipimo kama ujauzito upo) wala kuuliza historia ya mgonjwa.

Utafiti uliofanyika ulionyesha uwepo wa nyumba na vyumba vya kupanga vinavyotumiwa kwa shughuli hizo.

Katika eneo la Yombo, mkazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema wanawake vijana huonekana kuingia katika nyumba moja nyakati za jioni.

“Wengi huja usiku. Wakati mwingine unasikia mtu analia, lakini watu hatuulizani,” alisema.

Msimamizi wa moja ya nyumba ambayo wamepanga wanachuo iliyopo Sinza, alisema baadhi ya vyumba hutumika kwa shughuli hizo na waliopanga hukubaliana na wanaohitaji kuvitumia kwa shughuli hiyo kwa malipo maalumu.

“Unakuta wanakuja wanaingia ndani. Aliyepanga utaona anatoka, wageni wake watakaa kwa dakika 20 hivi, kisha wanaondoka. Wengi hawaulizi, mradi kodi imelipwa,” alisema.

Uchunguzi huo pia ulibaini baadhi ya maduka ya dawa yanayotajwa kama sehemu rahisi ya kupata dawa zinazotumika kutoa mimba bila kufuata taratibu.

Katika famasi mojawapo iliyopo Tabata Segerea, mwandishi alipouliza kuhusu dawa maarufu misoprostol alitajiwa bei ya Sh60, 000. Wiki moja baadaye kwenye famasi nyingine Kinondoni alitajiwa bei ya Sh150, 000 na huko kote hakudaiwa cheti cha daktari.

Wafanyakazi wa maduka ya dawa waliokubali kuzungumza bila kutajwa majina, walisema mahitaji ya dawa hizo kwa sasa ni makubwa.

“Wasichana wengi wanaogopa kwenda hospitali kwa sababu ya aibu na kuhukumiwa,” anasema mmoja wao.

Hata hivyo, madaktari wa afya ya uzazi wanaonya kuwa matumizi holela ya dawa hizo yanaweza kusababisha madhara makubwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama katika Hospitali ya Misheni Ifakara, mkoani Morogoro, Elias Kweyamba alisema misoprostol hutumika kusafisha kizazi ambacho mimba imeharibika kwa sababu zozote zile, kwa kutolewa au kutoka yenyewe.

“Pamoja na mifano hii ya moja kwa moja, ila matumizi yanatofautiana kulingana na hali ya mgonjwa na mtabibu atakavyoona inafaa, hivyo ni muhimu kuzitumia kwa ushauri wa daktari na si vinginevyo,” anasema Dk Kweyamba.

Wataalamu walisisitiza kuwa dawa hiyo haishauriwi kutumika kama njia za utoaji mimba mpaka pale daktari awe amemwandikia mgonjwa, kama anavyosema Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Ali Said.

“Wanaotumia dawa za kutoa mimba maarufu miso, wamekuwa wakikutana na changamoto ya kushindwa kukadiria umri wa mimba na vidonge vingapi atumie, hivyo wengi wanatoa mimba lakini haitoki kikamilifu na wengine kuvuja damu nyingi,” anasema Dk Said, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo cha Sayansi na Afya Shirikishi (Muhas).

Simulizi za manusura

Kwa Naomi, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 19 wa jijini Dar es Salaam, tukio hilo lilimwacha katika hali ya hofu kubwa.

“Nilidhani ni jambo rahisi kwa sababu waliniambia ni dawa tu. Lakini baadaye nilianza kuvuja damu nyingi na nilihisi kama nakufa,” alisema.

Alisema aliokolewa baada ya kupelekwa hospitali na rafiki zake.  “Daktari aliniambia ningechelewa kidogo tu, maisha yangu yangekuwa hatarini.”

Neema, mwenye miaka 24 yeye alisema alipata maumivu na damu kidogo lakini hakwenda hospitali, “Niliogopa watu kujua. Nilikaa ndani siku mbili kisha hali ikawa kawaida.”

Asha, mwenye miaka 27, alisema licha ya kutopata madhara makubwa ya mwili, alibaki na hofu kwa muda mrefu, “Nilikuwa na mawazo mengi nikihisi labda nimeharibu kizazi sababu ilipita miaka mitatu mfululizo bila kushika tena mimba. Nilipoenda kwa daktari alinipima na kuniambia mirija yangu ilikuwa imepata shida akanitibu.”

Akitaja athari zake, Dk Kweyamba alisema hospitalini hupokea wasichana na wanawake wenye kutokwa damu nyingi, maambukizi makubwa na mimba zisizotoka kikamilifu.

“Baadhi yao hufika wakiwa katika hali mbaya sana. Wengine wanachelewa kufika hospitali kutokana na hofu au aibu,” alisema.

Hata hivyo baadhi ya wauguzi ambao hawakutaka majina yao kutajwa, walisema familia nyingi huficha chanzo cha tatizo au wagonjwa kwa kutoa taarifa zisizo kamili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), utoaji mimba ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia vifo vya wajawazito duniani.

Pengo la sera lachochea

Mfamasia Mwandamizi wa Baraza la Famasia, Aloyce Gregory anasema pengo la sera kati ya hospitali na famasi za jamii limechangia kuongezeka kwa utoaji wa dawa zinazohitaji cheti, bila kufuata utaratibu.

Anasema Serikali ilizuia hospitali, hasa za umma, kutoa hati za kwenda kununulia dawa nje huku ikiendelea kusajili famasi za jamii kuhudumia wananchi. Hali hiyo, amesema, imekatiza uhusiano kati ya daktari na mfamasia.

“Kitendo cha kutoa dawa bila cheti cha daktari, sisi tunakiita utovu wa maadili ya kitaaluma,” anasema.

Gregory anasema famasi nyingi zinajikuta zikitoa dawa bila cheti kutokana na wananchi kuhitaji huduma wakati prescriptions (cheti cha dawa) hazitolewi kirahisi hospitalini.

Anasema Baraza linaendelea kufanya ukaguzi wa kawaida na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wataalamu watakaobainika kukiuka taratibu.

Hata hivyo, anasema udhibiti wa dawa sokoni na ufuatiliaji wa matumizi yake ni jukumu la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Meneja Kitengo cha Uhusiano kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Gaudensia Simwanza amesema: “Tunahusika na ukaguzi wa ubora wa dawa kama kuna dawa bandia au duni, lakini kwenye uuzaji ni Baraza la Famasia ndiyo linalosimamia, maana wafamasia wanakula kiapo kupitia Baraza, suala la maadili wanaofanya ni wenzetu wa Baraza.”

Sheria, hofu na sintofahamu

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu nchini, utoaji mimba unaruhusiwa tu pale unapolenga kuokoa maisha ya mama.

Wakili wa kujitegemea Peter Majanjala amesema sheria za Tanzania bado zinakataza utoaji mimba isipokuwa katika mazingira mahsusi ya kuokoa maisha ya mama, huku akibainisha kuwa kifungu cha 150 cha Kanuni ya Adhabu kinahusu mtu anayesababisha mimba kutoka kwa kutumia dawa, vifaa au njia nyingine.

Amesema licha ya uwepo wa vifungu vinavyoruhusu huduma katika mazingira maalumu, bado sheria haijahalalisha utoaji mimba kwa ujumla.

Majanjala anaeleza kuwa sintofahamu katika tafsiri ya sheria imeongeza hofu kwa watoa huduma za afya na wanawake wanaohitaji msaada.

Anasema mazingira hayo yamechochea kuibuka kwa mtandao wa siri wa utoaji mimba usio na usimamizi wa kitaalamu au wa kisheria.

Ameongeza kuwa wanawake wengi huogopa kukamatwa au kunyanyapaliwa hivyo kuchelewa kutafuta matibabu baada ya mimba kuharibika.

Pia amesema baadhi ya masharti ya Itifaki ya Maputo bado hayajaingizwa kikamilifu kwenye sheria za ndani, jambo linaloacha pengo la kisheria kwa waathirika wa ubakaji, ukatili wa kingono na changamoto za afya ya akili.

Inaendelea…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *