
Wakaazi wa Goma, Mashariki mwa DRC sasa wanakabiliwa na mzigo mzito wa kuendelea kukabiliwa na ugumu wa maisha kutokana na kutatizika kwa shughuli za kibiashara, na sasa maambukizi ya virusi vya Ebola yameongeza hofu.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika soko la Alanine, wauzaji wanasema biashara imepoteza mwelekeo na wateja wamepungua. Nzigire, Mkaazi wa Goma anayeuza nyanya, anasema biashara imeathirika vibaya haswa wakati huu mlipuko wa Ebola ukiripotiwa.
“Nyanya huja hapa kutoka Rwanda kupitia mpakani lakini kwa sasa hali imebadilika kwa sababu ya Ebola na hata bei yake imepanda. Hali hii inatugusa sana . Ombi letu nikufunguliwa kwa mpaka tena ili kazi zetu ziendelee.”
Uongozi wa waasi wa AFC-M23, wanaodhibiti mji wa Goma, umesema wameanza kuchukua hatua za kukabiliana na janga hilo. Miongoni mwa hatua hizo ni kampeni za kueneza uelewa kuhusu maambukizi, na uwekaji wa mabomba ya maji katika maeneo ya umma, hasa sehemu za kuingilia watu kama masoko na maeneo ya kukusanyika.
Kusitishwa kwa biashara za mipakani kwenye mpaka wa congo na nchi jirani ya Rwanda kwa sababu ya mlipuko wa Ebola kumesababisha kupanda kwa bei za bidhaa za msingi. Wauzaji na wakazi wanasema kuwa ugonjwa huu wa Ebola umeweka familia nyingi katika hali ngumu ya kiuchumi.
“Pamoja na mgogoro unaoikumba mji wa Goma kati ya serikali ya kongo na waasi wa M23 hali ya maisha imekuwa vibaya sana hasa pale Ugonjwa wa Ebola ulipotangazwa katika mji huu “.
Wataalamu wanasema mlipuko huu unahusisha aina mpya ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo. Hii ni aina ambayo kwa sasa haina chanjo maalum wala tiba ya kipekee.
