
Morogoro. Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) kimeanza utekelezaji wa miradi mipya 12 ya utafiti ya thamani ya Sh3.4 bilioni yenye lengo la kukuza maarifa na kutatua changamoto kwenye sekta ya kilimo, mifugo, mazingira na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda wakati wa mahafali ya 47 ya chuo hicho ambapo jumla ya wahitimu 877 walitunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo, Jaji Joseph Warioba.
Amesema kuanza kwa miradi hiyo kumefanya chuo hicho kufikisha miradi ya utafiti 130 inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Chuo kimeendelea kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti zinazofanywa na watafiti wa chuo hicho ili kuchangia sera na mipango ya Taifa,” amesema Profesa Chibunda.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Sua, Andrew Masawe amesema baraza limeendelea kutekeleza mambo yaliyolenga kuboresha sura ya chuo ikiwemo kusimamia matumizi bora ya fedha na ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema pamoja na mambo mengine, wameendelea kuhimiza utengenezaji na ukarabati wa miundombinu ya chuo kupitia mapato ya ndani, jambo ambalo limetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na miradi hiyo ya ukarabati ikiendelea vizuri.
Mmoja wa wahitimu wa shahada ya umahiri ya usimamizi wa habari na maarifa, Calvin Gwabala amesema chuo hicho ni kitovu cha kuzalisha wataalamu katika taaluma mbalimbali.
Hata hivyo, amesema kupata shahada katika chuo hicho sio lelemama kwa kuwa kipo kwa ajili ya kuandaa wataalamu watakaokuwa na uwezo wa kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
