Ni Chama tena SimbaNi Chama tena Simba

Miongoni mwa wachezaji wa Simba kwa sasa, hutoacha kulitaja jina la nyota wa kikosi hicho, Clatous Chota Chama ‘Triple C’, baada ya kuirejesha tena timu hiyo kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kusota kwa muda mrefu.

Asisiti mbili za mabao ya Libasse Gueye dakika ya 36 na la Alain Anicet Oura dakika ya 44, yametosha kuipa timu hiyo ushindi wa 2-1, dhidi ya Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini, Tanga na kumfanya Chama aibuke tena mchezaji bora wa mchezo kwa mara ya tano mfululizo.

Coastal Union ilianza kuishtukiza Simba kwa bao la dakika ya nane tu lililofungwa na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Maabad Maulid aliyekutana na mpira ukizagaa katika lango la timu hiyo ya Msimbazi na kupiga shuti kali la moja kwa moja.

Hata hivyo, Simba ilijibu majibu hayo kwa kutengeneza mashambulizi katika lango la Coastal Union, ambapo ilipata bao la kwanza kupitia Libasse Gueye, kisha, Anicet Oura akaandika la pili kwa kichwa akimaliza mpira wa kona ya Clatous Chama.

Mabao hayo mawili ya Simba yametokana na ustadi mzuri wa Chama ambaye tangu amerejea ndani ya kikosi hicho Januari 2026, akitokea Singida Black Stars, tayari amehusika katika mabao 12 ya Ligi Kuu Bara.

Chama aliyerejea msimu huu kwa mara ya tatu katika kikosi hicho, kiujumla amehusika katika mabao 14, akifunga sita akiwa na Simba na mawili akiifungia Singida Black Stars, huku akitoa asisti sita zote akicheza timu hiyo ya mitaa ya Msimbazi.

Kwa upande wa Libasse Gueye aliyejiunga na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, amefikisha bao lake la sita la Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, ikiwa ni mwendelezo mzuri tangu asajiliwe kikosini.

Kwa Anicet Oura raia wa Ivory Coast aliyejiunga pia na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2026, akitokea IF Gnistan ya Finland, ameendeleza kiwango kizuri tangu ajiunge na kikosi hicho, baada ya kufikisha bao lake la nne msimu huu la Ligi.

Bao la mshambuliaji wa Coastal Union, Maabad Maulid limemfanya pia nyota huyo kufikisha mabao sita ya Ligi Kuu msimu huu akiwa ndiye kinara wa kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’ akiivunja rekodi yake ya msimu uliopita aliofunga mabao matano.

Ushindi huu kwa Simba unaifanya timu hiyo kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 55, baada ya kucheza mechi 24, ambapo kati ya hizo imeshinda 16, ikitoka sare saba na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 44 na kuruhusu 10.

Simba imerejea kileleni kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho ilipoifunga Namungo ‘Wauaji wa Kusini’ mabao 3-0, Oktoba 1, 2025, ikiishusha Yanga kwa muda, ambayo leo itaikaribisha Singida Black Stars, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.

Yanga iliyokaa kileleni kwa muda mrefu ikipishana na maafande wa JKT Tanzania na Mbeya City kabla ya timu hizo kuishiwa nguvu mwishoni, kwa sasa iko nafasi ya pili na pointi 54, ikishinda mechi 16, sare sita na kupoteza moja tu kati ya 23.

Kwa upande wa Coastal Union, inaendelea kubakia nafasi ya 12 na pointi 25, ikishinda mechi sita, sare saba na kupoteza 11, ikiendeleza rekodi mbovu dhidi ya Simba katika Ligi Kuu, tangu mara ya mwisho iliposhinda bao 1-0, Machi 23, 2014.

Mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni Aprili 2, 2026, ambapo Simba ilishindi kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ dakika ya 25 na beki wa kati, Ismael Olivier Toure aliyefunga dakika ya 45+2.

JKT yabanwa jeshini

Katika mechi ya mapema iliyopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini, Dar es Salaam, wenyeji maafande wa JKT Tanzania waliambulia pointi moja, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Fountain Gate.

Fountain Gate ilianza kupata mabao yake kupitia kwa Juma Issa Abushiri dakika ya 3 na Ismail Aziz Kader dakika ya 45, kisha JKT ikajibu mapigo kupitia kwa Salehe Karabaka dakika ya 54 na bao kali la kideoni la Paul Peter dakika ya 86.

Matokeo hayo yameifanya JKT kufikisha pointi 37, ikiwa nafasi ya sita baada ya kushinda mechi tisa, sare 10 na kupoteza tano, huku Fountain Gate ikishika nafasi ya 11 na pointi 26, kufuatia kushinda saba, sare tano na kupoteza 12 kati ya 24.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *