Dar es Salaam. Mtuhumiwa Stephane Ngoie, aliyekuwa akitafutwa kwa takribani miaka mitatu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), amekamatwa na kurejeshwa nchini kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayomkabili ya tuhuma za kutapeli Sh1.6 bilioni.
Akizungumza leo Ijumaa Mei 22, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Kinondoni, Christian Nyakizee amesema mtuhumiwa huyo amerejeshwa nchini baada ya kukamatwa Uganda.
Mtuhumiwa Stephane Ngoie, akiwa amewasili nchini katika uwanja wa ndege aa Kimataifa wa wa Mwalimu Julius Nyerere(JNIA),baada ya kukamtwa ma maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) nchini Uganda
Amesema Ngoie, ambaye anadaiwa kutumia jina la Thomas Maweja katika shughuli zake za kihalifu, anakabiliwa na mashtaka pamoja na wenzake sita, katika Shauri la Jinai namba 12/2023 linalosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kwa mujibu wa Nyakizee, washtakiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na utakatishaji wa fedha haramu.
Mzigo wa chupa za vinywaji zilizokuwa zimeuzwa na Stephane Ngoie na wenzake kama madini ya Shaba.
“Kwa pamoja, washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Dola za Marekani 678,810 (Sh1.6 bilioni) baada ya kampuni yao ya Steca Export Company Limited kuuza ‘tani 110 za madini ya shaba’ kwa kampuni ya nchini China iliyopo Shanghai.
“Hata hivyo, badala ya kusafirisha madini hayo kadri ya makubaliano, washtakiwa hao walisafirisha makontena matano yaliyokuwa yamejazwa chupa tupu za vinywaji vilivyotumika,” alisema Nyakizee.
Ameeleza kuwa Ngoie ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, alikamatwa Aprili 2026 Entebbe nchini Uganda, baada ya kufuatiliwa kwa muda mrefu tangu mwaka 2023 alipotoroka Tanzania kukwepa uchunguzi na hatua za kisheria.
Kuhusu tukio la kitapeli walilolifanya, Nyakizee amesema lililotokea mwaka 2022 na baada ya uchunguzi wa Takukuru kukamilika, washtakiwa sita walifikishwa mahakamani huku Ngoie akiwa ametoroka tangu Mei 2023.
Mzigo wa chupa za vinywaji zilizokuwa zimeuzwa na Stephane Ngoie na wenzake kama madini ya Shaba.
“Takukuru kwa ushirikiano wa vyombo vya uchunguzi vya ndani na Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), iliendelea kufanya juhudi za kumtafuta mshtakiwa Ngoie katika nchi mbalimbali alizokuwa akienda ikiwemo Uganda, Kenya, Uturuki na China, kabla ya kubainika na kukamatwa Entebbe, Uganda Aprili 2026,” amesema.
Kwa mujibu wa Nyakizee, mtuhumiwa huyo ambaye ni raia wa Congo atafikishwa mahakamani kuunganishwa na washtakiwa wengine mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Mkuu huyo wa Takukuru amesema kwamba hakuna mtuhumiwa atakayekuwa salama popote atakapojjficha, iwe ndani au nje ya nchi.
Mkuu wa Takukuru Kinondoni Christian Nyakizee, akizungumza na waandishi wa habari.
“Serikali ya Tanzania haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahalifu wote, wawe raia au wasio raia, watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyokiuka sheria za nchi,” amesema.
