Arusha. Katika kukabiliana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira nchini, Serikali imezitaka sekta binafsi kuongeza nguvu katika ubunifu wa teknolojia za urejelezaji taka ili kuziwezesha kuwa bidhaa zenye thamani ya kibiashara sokoni.
Wito huo unatolewa wakati takwimu za Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zikionesha kuwa Tanzania huzalisha kati ya tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka ngumu kila mwaka, ambapo chini ya asilimia 50 pekee ndiyo hukusanywa rasmi na ni kati ya asilimia tano hadi 10 tu ya taka hizo zikirejelewa kwa sasa.
Kwa mujibu wa NEMC, pengo hilo kubwa la urejelezaji linaendelea kuchangia ongezeko la uchafuzi wa mazingira, kuziba mifereji ya maji mijini, kuongezeka kwa magonjwa ya milipuko pamoja na uharibifu wa mandhari ya miji.
Akizungumza leo Mei 22, 2026 katika maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani yaliyofanyika jijini Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali inaona teknolojia za urejelezaji ndio nguzo muhimu ya baadaye katika usimamizi stahimilivu wa taka na ulinzi wa mazingira.
“Kupitia ubunifu wa teknolojia zinazoweza kubadili taka kuwa bidhaa muhimu kama mbolea, nishati mbadala, vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku, ndio itakayosaidia nchi kuwa na usimamizi stahimilivu wa taka.
“Tunahitaji ushirikiano zaidi wa ubunifu wa sekta binafsi katika kubadili taka kuwa fursa za kiuchumi, na hii itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira lakini pia kuongeza ajira kwa vijana wetu,” amesema.
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Toba Nguvila amesema kwa sasa wanatoa elimu ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira ili kuvutia pia idadi kubwa ya watalii.
“Pia, tunafanya kampeni mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi hasa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema.
