DC Itunda awapongeza wauguzi Mbeya, awaasa kuendelea kuwa wawajibikajiDC Itunda awapongeza wauguzi Mbeya, awaasa kuendelea kuwa wawajibikaji

Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewapongeza wauguzi huku akiwaasa kuendelea kuwa wawajibikaji katika kutoa huduma bora za afya.

Itunda ameyasema hayo leo Mei 22, 2026 aliposhiriki Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya, ambapo tukio hilo lilihudhuriwa na wataalamu wa afya, viongozi mbalimbali pamoja na wananchi.

Katika maadhimisho hayo, Itunda ameeleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wauguzi waliojitokeza kusherehekea siku yao, akisisitiza kuwa wauguzi ni uti wa mgongo wa huduma za afya kutokana na mchango wao mkubwa katika kuhudumia jamii.

Itunda alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika kuimarisha miundombinu ya afya, upatikanaji wa vifaa tiba na kuboresha mazingira ya kazi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Itunda alibainisha kuwa juhudi za Serikali zimeleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya, na sasa wananchi wengi wanapata huduma kwa urahisi zaidi hata katika maeneo ya vijijini.

Maadhimisho hayo yamekuwa na tija kwa kuongeza hamasa na morali kwa wauguzi, huku akitoa wito kwao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na moyo wa kujitolea ili kuendeleza mafanikio ya sekta ya afya nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *