Tanzania nchi ya utamaduni wa latestTanzania nchi ya utamaduni wa latest

Dar es Salaam. Saa nyingine ukiiangalia jamii yetu kwa ujumla utagundua haipendi kujua historia yake. Kwenye jamii ya muziki kuna mambo mengi ambayo hunadiwa kama ni mapya, lakini hakika mengi ni marudio tu, ila historia haikuwekwa.

Nianze na upenzi mkubwa wa muziki wa Amapiano kutoka Afrika ya Kusini, hakika kwa sasa muziki huu umejikita vizuri kote nchini, si mjini na si vijijini, haipiti nusu saa lazima chombo cha utangazaji kimoja au kingine kitapiga wimbo wa Kitanzania ambayo umepigwa katika mahadhi ya Amapiano. Na mbaya zaidi mara nyingine wimbo umeigwa kila kitu kasoro lugha. Ukipita mitaani utasikia Amapiano toka kwenye ehemu za biashara na kwenye nyumba za watu binafsi. Kuna wadau wengine wa muziki ambao wameanza kulalamika kuwa aibu hii ya kukopi staili za nchi nyingine imezidi mno.

Kwa wanaofuatia historia ya muziki wa Tanzania kinachofanyika ni marudio tu ya hadithi ya zamani katika kitabu kipya. Kabla ya Uhuru na miaka kadhaa baada ya Uhuru, muziki wa Jive kutoka Afrika ya Kusini ulikuwa maarufu sana hapa nchini kwetu, umaarufu wake ulikuwa mkubwa kiasi cha kwamba karibu kila shule ilikuwa na kundi la Jiving, vijana waliimba nyimbo za Kizulu bila hata kujua maana yake. Mwanamuziki maarufu, Mbaraka Mwinyshehe alianza safari yake ya muziki kwa kuwa mpiga filimbi aliyekuwa akipiga kwa staili ya jiving. Alijiunga Morogoro Jazz Band kama mpiga filimbi wa staili ya jiving.

Ukiangalia katika muziki wa dansi pia huko kizazi kipya cha wapiga madansi, kinajitahidi kwa nguvu kuiga kila kitu kutoka kwa wanamuziki wa Kongo. Vijana wanaiga kila kitu mpaka aina ya nguo za kuvaa na hata kujichubua na kufuga ndevu. Siku hizi ukizunguka miji mikubwa nchi nzima bendi zinapiga muziki unaofanana, na kuvaa mavazi yanayofanana, huku ‘wacheza show’ wao wakiwa wanacheza kwa mitindo inayofanana inayotoka Kongo, sasa jambo hili linaonekana ni ubunifu mpya.

Hebu turudi nyuma miaka 50 hivi. Hali ilianza kuelekea kuwa kama sasa, wanamuziki wa muziki wa dansi walianza kuiga kila kitu kutoka Kongo. Wimbo ukitolewa na bendi ya Kongo, unadakwa juu juu na kuigwa na bendi zilizokuwa hapa nyumbani. Ilifikia mpaka bendi mbili au zaidi kuiga wimbo mmoja na kuurekodi. Bendi moja ikafikia mpaka kutunga wimbo wenye maneno yafuatayo’

‘Koma koma koma kaka wewe tunga zako’.

Uigaji wa Ukongo ulifika hatua mpaka Vijana Jazz Band kutunga wimbo wa kukemea waliokuwa wakiiga mno wanamuziki wa Kongo. Baadhi ya maneno ya wimbo huo yalikuwa haya;

‘Ohh ni mwanaume gani ana suka nywele?

Ohh nimwanaume gani anapaka wanja?

Ohh ni mwanaume gani anapaka Ambi?’

Ambi ilikuwa krim maarufu ya kuchubua ngozi, tena ilikuweko Ambi for Men maalumu kwa ajili ya Ngozi ngumu ya wanaume.

Kutokana na kutojua historia nimeshawahi sikia watu wakilalamika, ‘Ohh vijana wa kiume siku hizi nao eti wanajichubua.’ Hilo halikuanza leo, waliokuweko walitungiwa mpaka nyimbo.

Kabla ya katikati ya miaka ya 80, bendi nyingi zilikuwa hazisambazi na kuuza nyimbo zake na bendi zilitegemea kurekodi nyimbo kwenye studio za RTD na baada ya hapo nyimbo hizo kupigwa redioni kama matangazo ili bendi ijulikane. Kipato kilitokana na viingilio vya maonyesho yaliyofanywa na bendi katika kumbi mbalimbali. Ujio wa teknolojia ya kaseti ulitoa uwezo wa kuanza kuuza nyimbo kwa mtindo wa ‘album’. Wasambazaji wa kazi hizi walikuwa wengi, walikuweko wasambazaji maarufu kama Congo Corridor, Japanese Doll, Mamuu Stores, FM Productions, Musicland na kadhalika. Biashara hii iliendelea mpaka katikati ya miaka ya 2000, na kupotea taratibu kutokana na mchanganyiko wa sababu. Wasanii wakaanza kutoa ‘single’. 

Nia ya kutoa ‘single ilikuwa ni kutafuta nafasi wimbo upigwe kwenye redio ili wadau wausikie, ili msanii apate nafasi ya kualikwa kwenye maonyesho, wenyewe wakaanza kuuita mtindo huo ni latest ambao nia ni kibiashara zaidi, hawakujua kuwa kabla ya ujio wa biashara ya kuuza  na kusambaza kaseti, huo ndio ulikuwa mtindo wa wahenga wao.

Siku moja niliwahi kumsikia msanii wa Bongo muvi akidai kuwa yeye ndie Mtanzania wa kwanza kutoa filamu kamili. Nikawaza bahati mbaya sana hajui historia ya filamu. Angejua kuwa kulikuwa na Watanganyika walicheza filamu za komedi miaka ya 50 asingefungua mdomo. Mzee gani wa zamani aliyekuwa hamfahamu Mhogo mchungu, yule wa miaka ya 1950?

Kuna maana sana kuwa na historia ya kila jambo, usipojua unakotoka unaweza kudhani kuwa unaenda mbele kumbe unarudi nyuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *