Kisa Rio… Mrisho Ngassa afufua kumbukumbu za SeattleKisa Rio… Mrisho Ngassa afufua kumbukumbu za Seattle

MARA nyingi matukio makubwa katika soka huacha kivuli ambacho huendelea kuishi kwa miaka mingi. Alhamisi ya Mei 20, 2026 jijini Dodoma, kivuli hicho kilijitokeza upya wakati ambapo Mrisho Ngassa alipokutana tena na nyota wa zamani wa Manchester United Rio Ferdinand.

Siku hiyo ilifungua ukurasa wa nyuma wa historia hadi Julai 2011 nchini Marekani ambapo Ngassa alipata nafasi ya kucheza dhidi ya Manchester United akiwa kwenye majaribio ya kujiunga na Seattle Sounders FC ya Ligi Kuu Marekani (MLS).

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa ulichezwa katika dimba la CenturyLink Field mjini Seattle ambapo Ngassa aliingia kipindi cha pili na kukutana moja kwa moja na mastaa wakubwa wa Manchester United, akiwemo Ferdinand, ambaye wakati huo alikuwa sehemu ya kikosi cha wageni waliokuwa kwenye ziara ya kimataifa.

NGASS 02

Wakati huo Manchester United ilikuwa chini ya kocha wake wa kihistoria Sir Alex Ferguson. Katika mchezo huo, United waliibuka na ushindi wa mabao 7-0 huku Wayne Rooney akifunga mabao matatu ‘hat-trick’.

Licha ya matokeo hayo kuwa mazito, siku hiyo ilibaki kuwa ya kipekee kwa soka la Tanzania, kwani Ngassa aliandika historia kwa kuwa miongoni mwa wachezaji wachache wa Kitanzania waliowahi kucheza dhidi ya moja ya klabu kubwa zaidi duniani katika enzi zake za ubora.

Safari ya Ngassa kwenda Marekani ilipata sapoti maalumu kutoka kwa Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kupitia michezo, utalii na maendeleo ya vipaji vya vijana.

NGASS 03

Kutoka Seattle 2011 hadi Dodoma 2026, wawili hao walikutana tena na Ngassa akamkumbusha Ferdinand tukio hilo lililotokea miaka 15 iliyopita. Ngassa pia anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa kwanza wa Kitanzania kufanya majaribio kwenye timu za Ligi Kuu England.

Mbali na mechi hiyo dhidi ya Manchester United akiwa na Seattle Sounders, Ngassa pia aliwahi kufanya majaribio ya kujiunga na West Ham United iliyokuwa chini ya kocha Gianfranco Zola, ingawa hakupata nafasi ya kusajiliwa rasmi.

Ferdinand alijijengea umaarufu mkubwa akiwa na Manchester United, ambapo alifanikiwa kushinda mataji sita ya Ligi Kuu England, Kombe la Ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa mwaka 2008, mafanikio yaliyomuweka miongoni mwa mabeki bora wa kizazi chake.

NGASS 05

Katika ngazi ya timu ya taifa, Ferdinand pia aliichezea England katika mashindano makubwa ya kimataifa ikiwemo Kombe la Dunia na Euro huku akijulikana kwa uwezo wake wa kusoma mchezo, kasi na utulivu uwanjani.

Katika mazungumzo yao ya Dodoma, ilielezwa kuwa Ferdinand alionesha furaha kukutana tena na Ngassa, wakikumbushia jinsi soka linavyounganisha watu kutoka mataifa tofauti kupitia historia na uzoefu waliowahi kushiriki uwanjani.

Alisisitiza pia umuhimu wa wachezaji wa Afrika kuendelea kuamini ndoto zao licha ya changamoto za safari za kimataifa.

NGASS 04

Kwa upande wake, Ngassa alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha vijana wa Tanzania kuwa safari yake ya Marekani na kukutana na Manchester United si tukio la kawaida, bali ni uthibitisho kwamba vipaji vinaweza kufika mbali endapo vitapewa nafasi na kuaminiwa katika majukwaa makubwa.

“Naamini katika ndoto na ndio maana leo kumbukumbu imetuunganisha, tumekutana tena baada ya miaka mingi, ilikuwa nafasi ya kipekee sasa ni wakati wa vijana wengine kuonyesha vile inawezekana wakiamini,” anasema nyota huyo ambaye aliwahi kutamba akiwa na Simba, Yanga na Azam. Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali, Ngassa ameacha alama kubwa katika historia ya Tanzania.

Takwimu zinaonesha kuwa amecheza mechi 100 za kimataifa (caps 100) na kufunga mabao 25, jambo linalomuweka miongoni mwa wachezaji bora wa muda wote wa taifa. Rekodi hizo zinamfanya Ngassa kama mmoja wa nguzo muhimu katika kizazi cha wachezaji kilichoiwezesha Tanzania kushiriki mashindano mbalimbali ya Afrika ikiwemo CECAFA.

NGASS 01

MSUVA AMVULIA KOFIA

Nyota wa klabu ya Al-Talaba SC, Simon Msuva amemzungumzia Ngassa kwa heshima kubwa, akimuweka miongoni mwa wachezaji walioweka msingi wa soka la Tanzania na kuonyesha njia kwa kizazi kipya cha wanasoka.

Msuva amesema Ngassa amekuwa chachu kubwa ya maendeleo ya wachezaji wengi vijana kutokana na mfano aliouonyesha uwanjani, hali iliyowafanya wengi kuanza kuamini kuwa inawezekana.

‘‘Ngassa ni mmoja wa wachezaji waliotufungulia njia. Alionyesha kwamba ndoto za soka zinaweza kufika mbali na alitupa hamasa sisi vijana kuamini kuwa tunaweza pia kufika kwenye viwango vya juu kimataifa,’’  amesema nyota huyo ambaye anacheza soka la kulipwa Iraq.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *