Ujenzi mpya maeneo yaliyobomolewa Kimara waibua mjadala, Tanroads yafafanuaUjenzi mpya maeneo yaliyobomolewa Kimara waibua mjadala, Tanroads yafafanua

Dar es Salaam. Miaka kadhaa baada ya operesheni ya bomoabomoa iliyofanyika kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro na kulinda hifadhi ya barabara katika maeneo ya Kimara jijini Dar es Salaam, baadhi ya wananchi wameanza kurejea na kufanya ujenzi wa kudumu.

Hali hiyo imeibua maswali miongoni mwa wananchi kuhusu usimamizi wa maeneo hayo, huku baadhi yao wakihoji iwapo kurejea kwa shughuli za ujenzi katika eneo hilo kunaweza kusababisha bomoabomoa nyingine au kuibua uvamizi mpya wa maeneo hayo.

Mbali na sintofahamu hiyo, wajasiriamali waliokuwa wakifanya biashara katika vizimba vya muda katika Soko la Kimara Temboni, lililopo kandokando ya barabara hiyo, wamedai kutelekezwa baada ya kuondolewa kwenye maeneo yao ya awali kwa maelezo kuwa, kulipatikana mwekezaji mpya anayetarajia kuwekeza.

Mwananchi imeshuhudia eneo lilipokuwa soko hilo likiwa limezungushiwa mabati kuonesha kuna ujenzi unatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Itakumbukwa kati ya mwaka 2017 eneo la Kimara lilikuwa sehemu ya operesheni ya bomoabomoa katika maeneo ya kando ya Barabara ya Morogoro, hasa kutoka Ubungo hadi Mbezi ikitarajiwa bomoabomoa kufika mpaka Kibaha mkoani Pwani.

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ilibomoa nyumba, biashara, makanisa, misikiti na miundombinu mingine iliyokuwa ndani ya hifadhi ya barabara ili kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro kuwa ya njia nane pamoja na mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT).

Katika bomoabomoa hiyo, inaelezwa maeneo mengi ya Kimara yalikuwa yamevamia hifadhi ya barabara kinyume cha sheria huku Tanroads ikibainisha sheria ya zamani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro iliyotungwa tangu mwaka 1932 ilikuwa inaweka eneo kubwa la hifadhi.

Wakati ule, Tanroads ilisema kati ya Ubungo na Kimara baadhi ya maeneo yalitakiwa kuwa mita 90 kutoka katikati ya barabara kila upande, na maeneo mengine hadi zaidi ya mita 120.

Hivi karibuni, baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na bomoabomoa katika barabara hiyo yameonekana kuzungushiwa uzio wa mabati kuonesha yapo kwenye hatua za ujenzi.

Mbali na uzio wa mabati kwenye baadhi ya maeneo, pia yapo yanayojengwa kuzungushiwa ukuta wa matofali ya saruji, hali iliyoibua sintofahamu kwa wananchi huku baadhi wakionesha wasiwasi juu ya udhibiti wa kutosha wa maeneo hayo baada ya bomoabomoa ya awali.

“Ujenzi umekuwa ukifanyika wa kudumu na usio wa kudumu, swali ni je? Hawa wanaojenga ujenzi wa kudumu katika maeneo ambayo awali yalibomolewa kwa kuwa,  yapo kwenye hifadhi ya barabara wanajiamini nini?,” amehoji mmoja wa watu waliobomolewa nyumba eneo la Kimara aliyeomba hifadhi ya jina.

Mkazi mwingine, Nashon Philimoni amesema katika maeneo yaliyobomolewa eneo la kimara kunahitajika udhibiti wa kutosha ili kuepusha uvamizi kwa mara nyingine.

“Watu wanajenga tena ujenzi wa kudumu, sifahamu kama wanaojenga wapo kisheria au ni uvamizi, tulishuhudia bomoabomoa kubwa na watu wengi kupata hasara, kinachoshangaza ujenzi unarudi kwa kasi na watu wanajenga uwekezaji wa kudumu,” amesema.

Mwananchi ilimtafuta meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Alinanuswe Kyamba kutaka kufahamu ujenzi wa kudumu kwenye maeneo hayo umeruhusiwa na hatma ya wanaofaya ujenzi wa kudumu kwenye maeneo hayo.

Akifafanua hilo, Kyamba amesema wapo wanaopangishwa ili kuweka vitega uchumi akisisitiza upangishaji huo ni wa muda wa mkataba wa mwaka mmoja na haupaswi kujenga kitega uchumi cha kudumu.

“Katika maeneo ya hifadhi ya barabara huwa tunapangisha kama hatuyatumii kwa wakati huo, ukiyaacha yanatengeneza vichaka na kuwa sehemu za uhalifu,” amesema na kuongeza.

“Tanroads huwa tunapopangisha tunawaambia ni kwa muda wa mwaka mmoja hicho ni kama chanzo cha mapato cha Tanroads, na aliyepanga anapomaliza mwaka kama bado hatulitumii anaomba kuendelea, kama tunalitumia basi anaondoka,” amesema.

Kuhusu wanaofanya ujenzi wa kudumu, Kyamba amesema hairuhusiwi na kubainisha kwamba kama kuna mtu anajenga ukuta katika eneo hilo, yeye kama meneja hajajua ni nani.

“Sipo Dar es Salaam, nipo Dodoma kwenye bajeti yapata wiki sasa, tukirudi wiki ijayo tutatembelea kukagua eneo hilo,” amesema na kufafanua kwamba hifadhi ya eneo lote la barabara hiyo inapaswa kuwa mita 121.

Kuhusu Soko

Mbali na ujenzi wa barabara, pia eneo lilipokuwa Soko la Temboni limezungushiwa mabati kuonesha ujenzi unaendelea huku wajasiriamali waliokuwepo awali wakilalamika kuondolewa kwa madai limepata mwekezaji na wao kutelekezwa kwenye eneo ambalo halina miundombinu muhimu.

Mwananchi ilishuhudia baadhi ya wajasiriamali wakikusanya mbao za vizimba vyao katika soko hilo, na wengine wakijenga vizimba vipya katika eneo ambalo wamedai kuhamishiwa pia ni pembezoni mwa barabara ambalo wanasema ni bondeni na nyakati za mvua eneo hilo lijaa maji.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Rehema Ally amesema walipohamishwa waliambiwa wanampisha mwekezaji, lakini eneo walikohamishiwa ni bonde ambalo kipindi cha mvua maji yanajaa na hata wateja hakuna kutokana na ugumu wa miundombinu bajaji kushindwa kuingia.

“Hapa kuna makundi manne ya wafanyabiashara, sisi wa biashara ndogo ndogo, bajaji, msuli moto (mchanga) na gereji, lakini miundombinu yake ni shida,” amesema.

Katibu wa waendesha bajaji eneo la Temboni,  Saimon Lupatu amesema walipoondolewa eneo hilo kupisha mwekezaji walikubali kwa kuwa waliahidiwa wanakohamishiwa pataboreshwa.

“Eneo ambalo tulikuwa tunafanyia kazi wamezungushia mabati, tumeondoshwa, hatujui hatma yetu ni nini,” amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dk Aron Titus Kugurumjuli alipoulizwa kuhusu soko hilo amesema kwenye eneo ambalo ni hifadhi ya barabara anayehusika ni Tanroads.

Hata hivyo, Kyamba alipoulizwa amesema masoko yapo chini ya Halmashaurina kama wapo waliojenga kwenye hifadhi ya barabara basi wanatakiwa watoke kwa kuwa ni wavamizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *