MIONGONI mwa kitu kilichobarikiwa kisiwa cha Pemba ni kuwa na utajiri wa michezo mbalimbali ya utamaduni yenye asili na maana kubwa, kitu cha kufurahisha zaidi wanarithishana vizazi kwa vizazi.
Vikundi vingi vya michezo ya utamaduni kisiwani hapa kilio chao kikubwa ni kipato ambacho hakikidhi mahitaji ya wasanii hao kuendesha familia zao.
Mwandishi wa makala hii amepata nafasi ya kuona mchezo unaoitwa Kiyumbizi unaopatikana katika kijiji cha Pujini kilichopo Mkoa wa Kusini Pemba na kupata ufafanuzi kutoka kwa msanii wa kikundi hicho, Hamad Bakari Haji. Mchezo huo una raha na burudani tosha hasa unapopata nafasi ya kushuhudia namna unavyochezwa kwani una mtindo wa kipekee wenye kugusa hisia za mtu moja kwa moja.
KWANINI KIYUMBIZI?
Mchezo huo ni wa asili na umetokana baada ya wazee wa enzi hizo kuonewa, katika kutafuta namna bora ya kujikomboa na hilo ndipo wakaamua kutafuta kiyumbizi.
Kiyumbizi ni neno ambalo lilitumika likiwa na maana kujikinga kwa kutumia fimbo ambazo zilitumiwa na wazee kila walipokutana kwa kupigana kwa lengo la kuondoa uonevu.
Msanii huyo anasema wazee hao walipokutana kwenye maeneo mbalimbali kila mmoja alitumia fimbo yake kumpiga mwenzake huku mwingine akijikinga kwa kutumia fimbo yake na baadaye kusalimiana na kuondoka.
SHERIA ZAKE NA UNAVYOCHEZWA
Anasema, sheria ya mchezo huo kwa hatua ya kwanza wanaingia uwanjani kwa kupigiwa ngoma inayoitwa umundi hadi wachezaji wa mchezo huo wanapomaliza kujipanga kuwa levo moja na kugusana kidogo kisha hurudi na ngoma hiyo kuzimwa. Wakati ngoma hiyo ikizimwa, inaanzwa nyingine ambayo ndio maalumu kwa kiyumbuzi na hapo ndipo unapoanzwa kuchezwa kwa kutumia fimbo.
Anasema, katika mchezo huo kuna aina tatu za fimbo ikiwemo mtataso, mbilimbili na nyinginyingi ambapo wasanii wanajua aina hizo wakati wa uchezaji wake.
Anaendelea kutupa sifa zinazohitaji kuwa nazo mchezaji wa mchezo huo mojawapo ni kujua aina zote za fimbo za mchezo huo, kupiga ngoma, uchezaji na utaratibu.
Anasema, mchezo huo huwezi kuucheza kabla ya kujifunza kuanzia ukamataji wa fimbo, namna ya kukaa wakati wa uchezaji na umaliziaji wake.
Anafafanua kuwa, fimbo za mchezo huo zinatakiwa kuwa ‘size’ ya kati ambazo sio ndefu wala fupi sana zinazoweza kukamatika na hazipaswi kukatika.
Kwa hiyo, zinakuwa ni mti maalumu ambao hauwezi kuvunjika kirahisi kwani wakitumia ambao mbovu utasababisha athari kwao.
Pia, anasema mchezaji wa mchezo hatakiwi kumpiga mwenzake sehemu aliyotumia kukamatia fimbo hiyo na ikitokea anaruhusiwa kumrejeshea maana amevunja sheria ya mchezo.
Vilevile, anasema mchezaji hapaswi kuichukua fimbo hiyo kwa kuinama ama kama anachukua kitu cha kawaida, fimbo inachukuliwa kwa kurushwa na mwingine anaidaka bila ya kuanguka.
Tahadhari inachukuliwa kwa wachezaji muda wote wa mchezo kwani hakuna mwenye uhakika wa sehemu ambayo fimbo hiyo itatua inapopigwa ingawaje uhakika uliopo ni kuwa itagonga fimbo ya mwenzake.
“Nina uhakika wa ninavyopiga itagonga fimbo ya mwenzangu, sitomuathiri kichwa, mkono wala mabega,” anasema.
MCHEZO WA STAREHE
Anasema huo ni miongoni mwa mchezo wenye starehe kubwa kwa sababu hata viongozi wenyewe baadhi yao hawawezi kuukosa wanapofanya matamasha yao.
Licha ya kupendwa kwa mchezo huo bado hakuna mchango wowote wanaoupata kutoka kwao kwani hawajawahi kufika kwao kuzungumza nao na kutatua changamoto zao.
CHANGAMOTO
Kinachoukwaza mchezo huo ni kutumia gharama na muda kufanya mazoezi kisha baada ya hapo wanapewa taarifa ya kutohitajika kwenye tamasha au shughuli.
Anasema, jambo hili linawaumiza sana wana kikundi kwani wanachama wake wengine wanatoka nje ya kijiji hicho, hivyo wanalazimika kutumia nauli zao bila mafanikio.
“Wakati mwingine tunapewa hadi nyimbo za kuimba na tarehe ya tukio lakini siku moja kabla inaletwa taarifa ya kuahirishwa au hatuambiwi chochote zaidi ya kusubiri bila kufika mwisho,” anasema. Anasema, changamoto nyingine kuwekwa nyuma kwenye shughuli bila ya kupewa kipaumbele, hivyo huwalazimu kupata mualiko kupitia mgongo wa mtu mwingine na sio wao moja kwa moja.
Anasema wao ndio wahusika kwa maana hiyo sio busara kupewa mialiko bila ya kufikiwa wenyewe kwa kupatana bei kwani hiyo ndio kazi yao ya kuendesha familia, hawapaswi kudharauliwa.
MAPENDEKEZO
Wanakikundi hicho wanatamani kutambulika rasmi kwa kupewa nafasi ya kujisimamia wenyewe.
“Tunahitaji taasisi au wadau wanaohitaji mchezo huu kuchezwa kwenye matamasha yao watufikie wenyewe tukubaliane bei, hatufaidiki na chochote,” anasema. Kikundi hicho kina jumla ya watu 20 kati yao wanawake saba na wanaume 13, ametoa wito kwa wanaotaka kujiunga na kikundi hicho wanakaribishwa.
Pia, wameiomba serikali kuwaunga mkono kwa lengo la kuuboresha mchezo huo na kuufanya kuwa na mafanikio zaidi.
