Mastaa Bongo wanavyogawana kipato na nduguMastaa Bongo wanavyogawana kipato na ndugu

Dar es Salaam. Katika kiwanda cha burudani, mafanikio ya msanii mara nyingi huonekana kupitia jukwaani, kwenye tuzo anazopata au hata idadi ya mashabiki alionao.

Wengi huamini safari ya msanii hujengwa na meneja, kampuni kubwa, lebo au marafiki wa karibu waliopo kwenye tasnia. Hata hivyo, nyuma ya pazia kuna nguvu nyingine ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwa baadhi ya mastaa wengi wa Tanzania ambayo ni familia.

Kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa kawaida kuona wasanii wakubwa wakifanya kazi kwa karibu na ndugu zao katika maeneo tofauti ya kazi zao.

Wapo wanaotumia ndugu kama wapiga picha, watayarishaji wa muziki, madj wa maonesho au hata watu wanaosimamia maudhui yao ya mitandaoni.
Miongoni mwao ni Burna Boy raia wa Nigeria ambaye alimteau mama yake mzazi Bose Ogulu kuwa meneja wake wa kusimamia kazi zake.

“Nilifanya hivyo kwa sababu mama yangu ndiye mtu ninayemuamini zaidi kwa hiyo kunisimamia ni jambo zuri zaidi pia mama yangu alikuwa tayari na uzoefu wa muziki kwani babu yangu Benson Idonije alishafanya kazi na akina Fella Kuti,” anasema Burna Boy kwenye moja ya mahojiano akijibu kwanini aliamua kumchagua mama yake kuwa msimamizi wake.

Wapo wengi mwingine ni mkali wa Afrobeats, Ayra Starr ambaye inaelezwa amekuwa akitunga ngoma zake pamoja na kaka yake Dami.Hapa Bongo wapo wengi na Mwananchi imekuchambulia baadhi yao.

ALIKIBA
Ni mmoja wa wasanii walioupa heshima kubwa muziki wa Bongofleva. Mkali huyo wa kibao cha ‘Finale’ aliyoshirikishwa na Bien mmoja wa kundi la Sautsol kutoka Kenya.

Kwanini kwa sababu ni msanii pekee Bongo ambaye ameshinda tuzo zaidi ya tano na kuwa kinara wa misimu miwili tofauti ya Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) akichukua mwaka 2016 tuzo sita na mwaka 2022 tuzo tano tofauti.
Miongoni mwa mastaa wanaoonekana wazi kutumia ndugu zake katika shughuli zake za muziki ni Ali Kiba ambaye katika matukio mengi amekuwa akisafiri na mdogo wake, Abou Kiba.Abou amekuwa mmoja wa watu wa karibu katika shughuli za AliKiba, hasa upande wa picha na maudhui ya matukio.
Picha nyingi za Ali Kiba zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii, kuanzia zile za jukwaani hadi matukio binafsi, mara nyingi hupigwa na mdogo wake huyo. Kwa wengi, hilo linaweza kuonekana kuwa jambo la kawaida, lakini ndani kuna taswira kubwa ya kuaminiana na kulinda brand ya familia.
Mbali na Abou mdogo wake mwingine Chicco Kiba ni meneja binafsi wa kaka yake Alikiba, Ikumbukwe hivi karibuni Mkurugenzi huyo wa lebo ya Kings Music alitangaza kuwa ameingia makubaliano na Benjamin Olwal raia wa Kenya katika kumsimamia kazi zake.

JUX
Mwaka 2008, Jux alisainiwa chini ya lebo ya A.M Records na kuanza kurekodi ngoma mbalimbali za R&B. Tangu wakati huo mkali huyo ameachia vibao mbalimbali vilivyopata umaarufu mkubwa.

Kwenye miaka 18 aliyofanya muziki wa Bongofleva ameachia albamu mbili ‘The Love Album’ iliyotoka mwaka 2019, albamu hiyo ilikuwa na ngoma maarufu kama ‘Sugua’, ‘Fashion Killer’ na nyinginezo alizowashirikisha wasanii kama Diamond Platnumz, Vanessa Mdee.
‘King Of Hearts’ aliiachia mwaka 2022 albamu hiyo ilikuwa na ngoma kama ‘Nidhibiri’ akimshirikisha Zuchu, ‘Lucky Now’ dhidi ya Bien na wengineo.
Mwanzoni Jux alikuwa akiwatumia baadhi ya waongozaji akiwemo Hanscana, Ivan & Jordan Hoechlin, na Justin Campos kwa baadhi ya video.
Hivi sasa msanii huyo amekuwa akifanya kazi kwa karibu na mdogo wake anayejulikana kama Mkambala Jr . Huyu ndiye anayehusika na baadhi ya video za promosheni na maudhui ya muziki wa Jux.
Sio kwa Jux pekee lakini pia hata kwa mama mkwe wake, muigizaji wa filamu za Nigeria, Iyabo Ojo amekuwa akifanya kazi na Mkambala Jr kwenye ubunifu wa video na picha mbalimbali.
Wapo wanaoamini kuwa mafanikio ya baadhi ya wasanii wa kizazi hiki yanachangiwa na namna walivyoweza kuunda timu imara zinazowajumuisha ndugu zao wa karibu.

PAULA KAJALA
Kwa upande wa binti wa muigizaji wa Bongo Movie, Kajala Masanja, Paula ni miongoni mwa wana mitandao wanaotumia vyema mitandao ya kijamii kuingiza maokoto kupitia matangazo.

Kupitia vlog zake zinazovutia mashabiki wengi mitandaoni zinazohusiana na maisha yake, mdogo wake anayefahamika kwa jina la Marasta ndiye anayehusika na upigaji picha na uchukuaji video wa maudhui hayo. Hili linaonyesha namna kizazi kipya cha burudani kinavyoona umuhimu wa kufanya kazi na watu wanaowaamini zaidi.
Kwenye moja ya mahojiano Paula anasema “Mdogo wangu ndiye alikuwa ananilazimisha tangu mwaka 2022 kuanzisha Vlog mimi nilikuwa naona kama siwezi akaniambia atanisaidia kwenye kuchukua video kwahiyo nikawa naangalia wengine wanafanyaje nje ndipo mwaka jana nikaamua rasmi kuanzisha.”
“Kwahiyo nilivyoanzisha nikamwambia yeye anisaidie kwenye mambo ya uzalishaji wa hayo maudhui kwa sababu niliamini ana uwezo mkubwa wa kunitengenezea na hata akikosea nina uwezo wa kumwambia.”

DIAMOND PLATNUMZ
Mwingine ni msanii na Mkurugenzi kutoka lebo ya Wasafi, Diamond Platnumz ambaye amekuwa akimtumia kaka yake RJ The DJ kama DJ wake kwenye shughuli zake mbalimbali za burudani.

RJ amekuwa na mchango mkubwa kwenye karia ya Diamond kwa muda mrefu tangu alipoanza kupata umaarufu mwaka 2010 kupitia ngoma ya ‘Kamwambie’ akiwa ndiye DJ wake katika maonesho na matukio mbalimbali.
Ukaribu wao umeonekana kuwasaidia kujenga maelewano makubwa jukwaani, jambo ambalo limekuwa faida katika maonesho ya kimataifa ya msanii huyo.
RJ anasema “Nikiwa kwa Simba mnanimbia mtegemea cha ndugu nikiwa peke yangu mnasema hatukuoni na Diamond, nafikiri watu wamekuwa na fikra nzuri sasa hivi na wengine wananipongeza RJ umekuwa ukipambana sana, kwahiyo tumefanya kazi nyingi sana na Diamond na mimi ni kaka yake familia kwahiyo tuna mengi.”

JAIVAH
Msanii mwingine ni Jaivah aliyepata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wa ‘Kautaka’. Katika safari yake ya muziki, mdogo wake anayejulikana kama Abbah Process amekuwa na mchango mkubwa katika utayarishaji wa muziki.
Hii ni ishara kuwa hata katika hatua za mwanzo za mafanikio, baadhi ya wasanii wanaona umuhimu wa kujenga mfumo wa kifamilia kabla ya kuingia kwenye lebo kubwa.

Jaivah anasema “Pale kuna mgawanyo mzuri wa kikazi hata pesa inajulikana inakwenda wapi hakuna shida wala migogoro kwa sababu sisi ndugu na tunafahamiana na tunakutana mara nyingi kwa hiyo kila mmoja anajua mgao wake.”
Pamoja na mastaa hao kushirkiana na ndugu zao kwenye kazi wapo baadhi wamekuwa kwenye migogoro isiyoisha wengi wamekuwa wakichanganya kazi na maisha binafsi.Tofauti na mfanyakazi wa kawaida, ndugu huwa sehemu ya familia na hilo linaweza kufanya baadhi ya maamuzi kuwa magumu.
Mfano wa ndugu waliofanya kazi kwa pamoja ni kundi la P Square linaloundwa na mapacha Peter Okoye na Paul Okoye ambalo lilianza kufanya kazi mwaka 2000 hadi mwaka 2017 lilipovunjika rasmi.
Taarifa zilieleza kuwa migogoro ilianza polepole, ikihusisha masuala ya uwazi wa mapato, maamuzi ya kibiashara na nafasi ya kila mmoja ndani ya kundi. Inadaiwa kuwa mmoja wa mapacha alihisi kunyimwa uhuru wa kufanya maamuzi ya ubunifu, huku mwingine akiona mfumo uliokuwepo ulikuwa sahihi kwa ukuaji wa biashara yao.
Hata hivyo, kwa mastaa wengi wa Tanzania wanaotumia mfumo huo, faida zimeonekana kuzidi changamoto. Wengi wao wameweza kujenga timu zinazodumu kwa muda mrefu tofauti na baadhi ya wasanii wanaobadilisha watu wa kazi mara kwa mara.
Kadri sekta ya burudani inavyokua, inaonekana wazi kuwa familia zinaendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya wasanii. Kutoka kwenye upigaji picha, utayarishaji wa muziki, maudhui ya kidijitali hadi maonesho ya jukwaani, ndugu wamekuwa nguvu kubwa nyuma ya pazia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *