Dk Mwinyi: Mjadala kuongeza muda wa uongozi hauna tijaDk Mwinyi: Mjadala kuongeza muda wa uongozi hauna tija

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema mjadala wa kubadili Katiba ili aendelee kuongoza Zanzibar kwa kipindi kingine hauna tija kwa Taifa.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi Zanzibar.

Amesema utaratibu wa hazina kutoa fedha kuendesha taasisi hizo umepitwa.

Rais Mwinyi amelazimika kutoa kauli hiyo kutokana na hivi karibuni kuwapo na mijadala kuhusu kuongezewa muda katika uongozi wake.

Akizungumza kuhusu hoja hizo leo baada ya kufungua Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi Zanzibar, Dk Mwinyi amewataka wanaoendekeza mjadala huo kuufunga kwani sio sehemu yake na kwamba wameapa kulinda Katiba ya nchi.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati akifungua jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi Unguja Zanzibar.

Dk Mwinyi amesema hata katika baraza la wawakilishi kumekuwa kukiibuka mjadala huo, wajumbe hao wana kazi kubwa ya kujadili mambo ya maendeleo.

“Sijui sababu yake nini, kwanza ndio tunaanza miezi sita tu tangu tumemaliza uchaguzi, maneno yameanza kuibuka, katika Baraza la Wawakilishi nayasikia, mitaani nayasikia, hata hapa msanii Kirobo amesema hayohayo,” amesema na kuongeza.

“Sisi tumeapa kuilinda Katiba ya nchi, kwa hiyo hatutaweza kufanya vinginevyo lazima tuilinde Katiba ya nchi. Lakini huu wasiwasi unatokana na nini mbona tuna miaka minne ya kufanya kazi?”

Rais Mwinyi amesema, “niombe Mwenyezi Mungu atupe uhai na uzima atuwezeshe kutekeleza majukumu yetu katika kipindi cha miaka minne na nusu ijayo, mimi nina matumaini makubwa kwamba nchi yetu itapiga hatua kubwa baada ya hapo tutapokezana vijiti na sina shaka, kwamba hapa tulipoanzia tutaendeleza safari ili nchi yetu ipate maendeleo kila mmoja wetu anayotarajia.”

“Kwa hiyo, mjadala huu sio wakati wake kabisa, hauna nafasi sasa. Kule baraza la wawakilishi kuna mambo mengi ya kujadili ya kimaendeleo, tuache jambo hili kwa kweli halina tija,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *