Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Waziri wa
Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amejaribu kuwahakikishia washirika wake
kuhusu maamuzi ya Marekani juu ya kupelekwa kwa wanajeshi barani Ulaya.
Kuingilia
kati kwa Rubio mwishoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Nato nchini
Sweden kulikuja baada ya Rais Donald Trump kusema kwamba Marekani itatuma
wanajeshi 5,000 zaidi nchini Poland.
Uamuzi huo
ulikuwa wiki moja baada ya mpango wa kupeleka wanajeshi 4,000 nchini humo
kufutwa na siku chache baada ya tangazo kwamba wanajeshi wa Marekani
wangeondolewa kutoka Ujerumani.
Matangazo
hayo yamesababisha mkanganyiko miongoni mwa washirika wa shirika la ulinzi la
trans-Atlantic. Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari baada ya
mkutano wa Nato siku ya Ijumaa, Rubio alisema Marekani ilikuwa ikitathmini upya
uwepo wake wa wanajeshi kila mara kwa kuzingatia ahadi zake za kimataifa.
Baadhi ya
wanajeshi wa Marekani kwa sasa wako Mashariki ya Kati, kufuatia mzozo wa
Marekani na Israel na Iran.
Trump alitoa
tangazo kuhusu kupelekwa kwa wanajeshi wapya Poland huku mawaziri wa Nato
wakiwa Sweden kwa mazungumzo.
Akiandika
kwenye jukwaa lake la Truth Social siku ya Alhamisi, Trump alisema uamuzi huo
ulitokana na uhusiano wa Marekani na Rais wa Poland Karol Nawrocki, ambaye
alimuunga mkono wakati wa uchaguzi wa rais mwaka jana na ambaye ni mfuasi wake
wa muda mrefu.
Kiongozi
huyo wa Marekani hakufafanua zaidi kama wanajeshi hao wa ziada walikuwa sehemu
ya mpango wa awali wa kupelekwa au operesheni tofauti.
