
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amemfuta kazi Waziri wake Mkuu, Ousmane Sonko, jioni ya Mei 22, 2026. Tangazo hilo lilitolewa kwenye kituo cha televisheni cha RTS muda mfupi kabla ya saa 6:00 usiku saa za Afrika ya Kati.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika hotuba fupi iliyorushwa muda mfupi kabla ya saa 4:00 kwa kwa saa za ndani siku ya Ijumaa, Mei 22 (Saa 6:00 usiku siku ya Ijumamosi), na shirika la Utangazaji la Senegal (RTS) kutoka Ikulu ya rais huko Dakar, Oumar Samba Ba, Katibu Mkuu katika ofisi ya rais, alitangaza kwamba Ousmane Sonko si Waziri Mkuu tena wa Senegal. Wajumbe wengine wa serikali pia walipoteza nafasi zao.
“Kwa amri nambari 2026-1128 ya Mei 22, 2026, Rais wa Jamhuri, Mheshimiwa Bassirou Diomaye Diakhar Faye, amesitisha majukumu ya Bw. Ousmane Sonko, Waziri Mkuu, na kwa hivyo, yale ya mawaziri na makatibu wa serikali ambao walikuwa wanachama wa serikali. Wajumbe wa serikali inayoondoka wanawajibika kushughulikia mambo ya sasa,” alisema Oumar Samba Ba.
Kufukuzwa kwa Ousmane Sonko kulikuja saa chache tu baada ya kuonekana kwake mbele ya Bunge la taifa, ambapo alijibu maswali kutoka kwa wabunge. “Mimi si Waziri Mkuu ambaye hutii na kukubaliana na kila kitu bila kujua,” Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema wakati wa kikao hiki. Katika tukio hili, pia alitaja “kutokubaliana” na rais, lakini hakuna kitu ambacho, kulingana naye, kilizuia utendaji kazi wa Serikali.
“Usiku wa leo nitalala kwa moyo mwepesi”
Mvutano ulikuwa ukiongezeka katika miezi ya hivi karibuni kati ya viongozi hao wawili, walioingia madarakani mwaka wa 2024, tofauti zao za kisiasa zikizidi kuwa wazi. Karibu wiki tatu zilizopita, katika mahojiano na waandishi wa habari, Bassirou Diomaye Faye alionyesha kwamba anaweza kumfukuza Waziri wake Mkuu ikiwa angepoteza imani naye. Hatua ambayo ameitekeleza usiku wa leo.
Kwa upande wake, Ousmane Sonko hakuchelewa kuzungumzia kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kufukuzwa kwake: “Usiku wa leo nitalala na moyo mwepesi,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mshauri wa zamani wa Bassirou Diomaye Faye na mpinzani wa rais wa zamani Macky Sall, Ousmane Sonko alikuwa amezuiwa kugombea katika uchaguzi wa urais wa mwezi Machi 2024 na alimteua mkuu wa sasa wa nchi kama mbadala wake.
“Sasa, pande zote mbili zitalazimika kutafuta mikakati inayofaa ili kuwepo na kubadilika ndani ya uwanja wa kisiasa kwa sababu, ingawa rais ana uwezo mkubwa[…], pia kuna mifumo ndani ya mfumo wa bunge ambayo inaweza kufanya kazi kwa faida ya Waziri Mkuu wa zamani Ousmane Sonko,” anasema Profesa Maurice Soudieck Dione, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Gaston-Berger huko Saint-Louis. “Kwa matarajio ya uchaguzi ujao—uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2027 na uchaguzi wa urais mwaka 2029—hatari ni kwamba tutashuhudia vita kati ya walio wengi kutoka kambi ya rais na walio wengi bungeni, hali ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya kwa utendaji mzuri wa masuala ya umma,” anaongeza Profesa Maurice Soudieck Dione.
