
BEKI wa kati wa Mbeya Kwanza, Vintani Mtega amesema bado hajajua hatima yake katika kikosi hicho baada ya mkataba wake wa sasa kufikia ukomo mwisho wa msimu huu wa 2025-2026, japo atapambana katika mechi zilizobakia kwa ajili ya timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtega amesema mkataba wake unaisha mwisho wa msimu huu na bado hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine, ingawa suala la kubakia au kuendelea kukichezea kikosi hicho itategemea na ofa mbalimbali atakazozipata.
“Malengo yangu kwa sasa ni kuipigania timu ili irudi tena Ligi Kuu Bara, kwa nafasi tuliyopo tunaweza kufanikisha hilo kutokana na ushirikiano tulionao kuanzia sisi wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kijumla,” amesema Mtega.
Nyota huyo aliyeanzia timu za vijana za Mbeya City kabla ya kujiunga na Mbeya Kwanza, amesema msimu huu umekuwa ni mgumu kutokana na ushindani mkubwa wa wapinzani wao, jambo linaloongeza ari kubwa ya kupambana katika kila mechi wanayoicheza.
“Moja ya jambo ninalofurahia ni kuona ninapata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza tofauti na msimu uliopita, hali hiyo inaniongezea morali ya kupambana kwa ajili ya kutimiza malengo ya timu tuliyoyaweka,” amesema Mtega.
