#HABARI: Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Serikali imeweka mkakati maalum wa kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linaendelea kuwa safi na lenye mazingira bora kupitia ushirikiano wa wananchi, taasisi binafsi, kampuni pamoja na wakandarasi wa usafi.
Mpogolo alisema hayo leo wakati wa zoezi la usafi lililoanzia eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Chuo cha Utumishi wa Umma, jijini Dar es Salaam.
Alisema katika kuimarisha usafi wa jiji hilo, kampuni, taasisi na viwanda vilivyopo kando ya Barabara ya Nyerere vimetakiwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha mazingira na usafi wa maeneo yao.
“Namtaka kila mmoja kuhakikisha anafika kwa mkurugenzi wetu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam au kutuma mwakilishi ili kwa pamoja tuweke mkakati wa kuhakikisha barabara yetu inakuwa safi na yenye mazingira bora,” alisema Mpogolo.
Alisema zoezi hilo ni sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani pamoja na mashindano ya AFCON, huku akisisitiza kuwa Dar es Salaam lazima ibaki kuwa safi muda wote.
Mpogolo alisema Halmashauri imeendelea kutenga maeneo maalum kwa wafanyabiashara ili kuondoa biashara holela zinazochangia uchafuzi wa mazingira na msongamano wa magari na watu barabarani.
“Tunataka Dar es Salaam ibaki kuwa safi wakati wote. Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kulinda mazingira kwa kuacha kutupa taka ovyo na kufuata utaratibu uliowekwa wa kufanya biashara,” alisema.
Aidha alisema Serikali imeanza kutumia vifaa vya kisasa vya usafi kwa ajili ya kuondoa michanga iliyosababishwa na mvua za masika katika maeneo mbalimbali ya jiji.
“Hivi karibuni tumetoka kwenye kipindi cha mvua za masika, hivyo kumekuwa na michanga mingi barabarani. Leo tumefanikiwa kuondoa zaidi ya tani nne za michanga na taka katika maeneo mbalimbali,” alisema.
Powered by #MCHEZOSUPA
JINSI YA KUSHIRIKI MCHEZO SUPA:
–
Tuma 1000 kupitia Airtel Money, Tigo Pesa, M – Pesa, Halopesa, kwenda namba ya kampuni 222223 kumbukumbu namba ni 777 au weka neno ITV.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
Follow @itvtz @radioonetanzania
(Feed generated with FetchRSS)
