Mahitaji ya huduma za intaneti yenye kasi kubwa yametajwa kuendelea kuongezeka nchini huku biashara, elimu na utengenezaji wa maudhui ya mtandaoni vikichochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kuwa usajili wa huduma za intaneti nchini umefikia milioni 58.9, sawa na kiwango cha matumizi cha asilimia 84.2 ya wananchi, huku huduma za mobile broadband zikibeba zaidi ya asilimia 58 ya matumizi yote ya intaneti nchini.
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema ongezeko hilo la matumizi ya teknolojia limeongeza mahitaji ya huduma za intaneti zenye kasi na uthabiti mkubwa kwa wananchi, wafanyabiashara na watengenezaji wa maudhui ya kidijitali.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Mahusiano wa TTCL, Ester Mbanguka, amesema biashara nyingi sasa zinafanyika mtandaoni huku watoa huduma na wafanyabiashara wakitegemea zaidi miundombinu ya intaneti kuwafikia wateja wao kwa haraka na kwa ufanisi.
Amesema watengenezaji wa maudhui mtandaoni pia ni miongoni mwa makundi yanayoongeza mahitaji ya intaneti yenye kasi kubwa kutokana na ongezeko la matangazo ya moja kwa moja, video za mtandaoni na biashara za kidijitali.
Kwa mujibu wa TCRA, matumizi ya data nchini yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 15 katika robo ya kwanza ya mwaka huu, yakifikia petabytes 932, ishara ya kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kidijitali na maudhui ya mtandaoni miongoni mwa Watanzania.
Mhariri @claud_jm
#AzamTVUpdates

(Feed generated with FetchRSS)