Dar es Salaam. Mwili wa Bhaozang Ge, mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI unaotarajiwa kuchomwa moto utashuhudiwa na ndugu wanne pekee, katika eneo maalumu lililotengwa sehemu ya Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mmiliki huyo raia wa China Bhaozang Ge (50), aliuawa na watu wanaodaiwa ni walinzi binafsi wa kiwanda hicho kilichopo Mabibo, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumamosi ya Mei 16, 2026 saa nane usiku.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 24, 2026, Msimamizi wa kiwanda hicho, Lucas Shao amesema ratiba iliyopangwa ni kuupeleka mwili wa Bhaoganza Ge kwenda eneo lililoandaliwa kwa ajili ya shughuli ya uchomaji katika eneo la Makumbusho.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Aristides Mbwasi akitoa salamu za rambirambi kwa familia alipofika kwenye eneo la msiba.
Shao amesema kwa mujibu wa ratiba waliyopewa, shughuli ya uchomaji itafanyika kwa saa mbili.
Amesema kwa kuzingatia utaratibu na mila za familia hiyo, watu watakaoruhusiwa kuingia katika eneo la uchomaji ni wanafamilia wanne pekee, huku waombolezaji wengine wakibaki nje wakisubiri shughuli hiyo kukamilika.
“Tumeambiwa tunaweza kwenda hadi Makumbusho lakini hatutashuhudia shughuli ya uchomaji, kutokana na utamaduni na mila zao, wanaoruhusiwa kuingia kushuhudia ni ndugu wa karibu ambao ni wanne,” amesema Shao.
Amesema watakaoingia ndani ni mke wa marehemu, mtoto wake, mdogo wake pamoja na ndugu mwingine wa karibu huku waombolezaji wengine wakisubiri nje hadi shughuli hiyo itakapomalizika.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Warejeshaji Taka Tanzania (Tara), Allen Kimambo amesema taifa limepata pigo kubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira na uwekezaji nchini.
Akizungumza kwa huzuni, Kimambo amesema marehemu alikuwa mtu aliyekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya mazingira, akipenda uwekezaji na kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na maendeleo.
“Tumepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa mstari wa mbele kusaidia sekta ya mazingira na uwekezaji, alikuwa mtu mwenye maono, aliyependa kuona jamii ikipata maendeleo kupitia kazi zake,” amesema Kimambo.
Kimambo amesema mchango wa marehemu haukuishia Tanzania pekee, bali uliwagusa watu wa ndani na nje ya nchi kutokana na moyo wake wa kusaidia na kujitoa kwa jamii.
“Msiba huu si wa hapa tu, ni msiba mkubwa hata kwa marafiki na wadau mbalimbali waliokuwa wakimuona kama nguzo muhimu katika maendeleo ya mazingira na uwekezaji,” amesema.
Kimambo amesema marehemu atakumbukwa kwa upendo wake kwa watu, kujali mazingira pamoja na namna alivyokuwa tayari kushirikiana na wengine kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali.
Amesema jamii inapaswa kuendeleza yale mazuri aliyoyaacha ili kuhakikisha ndoto na maono yake yanaendelea kuishi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi amesema wizara imeguswa na msiba huo na inaungana na familia, ndugu, jamaa pamoja na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
“Serikali kupitia wizara itaendelea kuwa karibu na familia katika kipindi hiki, huku akiwaombea faraja na uvumilivu wakati wa maombolezo,” amesema Mbwasi.
