Wazazi wanavyoua ubunifu kwa watoto wanapokoseaWazazi wanavyoua ubunifu kwa watoto wanapokosea

Dodoma. Umewahi kujiuliza kwa nini watoto wengi wanalalamikiwa kwa kukosa ubunifu?

Je, ubunifu wa mtu ni tabia ya kuzaliwa, matokeo ya malezi au mtu hujifunza shuleni? Hapa nazungumzia uwezo wa kulitazama jambo kwa kiu ya udadisi, kulitafutia majibu yasiyozoeleka.

Hata dhima kuu ya elimu iliyo bora ni kukuza ubunifu. Kama kuna kitu muhimu elimu bora humtendea mtu, kwa hakika, ni kumpanua uwezo wake wa kufikiri na kumuwezesha kuyatazama mazingira yake kwa jicho la kutafuta majibu yasiyofahamika.

Kinyume chake ni elimu inayorudia rudia yale yale ambayo, aghalabu, hayawezi kumsaidia mtu kukabiliana na changamoto mpya zinazojitokeza kila uchao.

Kazi za kiutafiti za ujifunzaji zinaonesha uhusiano mkubwa kati ya malezi na ubunifu. Miaka ya 1960 George Land na wenzake walifanya utafiti kupima uwezo wa watoto wa Kimarekani kufikiri kwa ubunifu.

Watoto hawa wa miaka kati ya minne na mitano walipewa jaribio linalopima uwezo wao wa kufikiri tatizo na kuja na majibu yanayoleta ufumbuzi wa changamoto.

Majibu yalionesha kuwa asimilia 98 ya watoto hao walionesha kiwango cha juu cha ubunifu. Land alibaini akili za watoto hawa wasioanza shule zilichemka kujaribu njia mbalimbali za kuja na majibu tofauti tofauti kumaanisha kuwa karibu kila mtu huzaliwa na ubunifu.

Jambo lililowashangaza Land na wenzake ni kwamba walipoingia shule, miaka mitano baadaye, watoto hawa walipopewa tena jaribio lilelile wakiwa na umri wa miaka 10, uwezo wao wa kufikiri kiubunifu ulishuka kwa takribani asilimia 68 na kufikia asimilia 30.

Hali ilikuwa mbaya zaidi watoto hawa walipokuwa na umri wa miaka 15. Ubunifu ulionekana kwa asilimia 12 pekee ya watoto ambao miaka 10 iliyopita,  walionesha kiwango kikubwa cha uthubutu na ubunifu.

Tuzungumzea kimalezi

Utafiti huu ukaleta tafsiri kubwa mbili kimalezi. Kwanza, kasoro ya ufundishaji. Inavyoonekana, shule zinachangia  kuua ubunifu wa watoto. Kadri mtoto anavyozoeshwa masomo shuleni na kuwa mwenyeji wa taaluma,  ndivyo anavyopoteza uthubutu wake na hivyo kufifiisha ubunifu wake. Hii ni habari mbaya kwa walimu na mfumo wa elimu. Hata hivyo, ukiwafuatilia watoto wetu wengi, unaona hili lina ukweli mkubwa.

Kuna namna watoto wakishaanza shule wanaanza kuishi kwenye maboksi ya matarajio ya walimu na kujikuta muda mwingi wanautumia kusoma, kukariri na kumridhisha mwalimu asiyetaka kusikia tofauti na kile anachokijua yeye.

Matokeo yake watoto wengi wanachagua kuwa ‘makasuku’ wa taaluma na kusahau maeneo mengine muhimu ya maisha. Hili la kwanza.

Lakini la pili, tunajifunza kuwa familia ni sehemu salama zaidi kulea ubunifu wa watoto kuliko shule. Unaweza kuona kabla mtoto hajaenda shule, mazingira ya nyumbani yanachangia kukuza uwezo wake wa kufikiri bila kulazimika kutafuta jibu linalofahamika na mtu mwingine.

Katika mazingira ambayo familia zinaruhusu uhuru wa kufikiri na mtoto anajifikia salama kujaribu, ni wazi hizo asilimia 98 zinaweza kupatikana.

Hata hivyo, ipo haja ya kuutazama utafiti huu kwa jicho tofauti kidogo kiutamaduni. Tujiulize, kwa mfano, utafiti huu ungefanyika kwenye mazingira yetu hapa nyumbani hali ingekuwaje ?

Je, asimilia ngapi ya watoto wa miaka minne hadi mitano hapa kwetu wangekuwa na kiwango cha juu cha ubunifu ? Ingawa hatuna utafiti tunaoweza kuurejea, lakini kuna ukweli kiasi fulani kuwa familia zetu zinachangia kuua uthubutu wa watoto kufikiri.

Fikiria namna tunavyowakosoa watoto. Fikiria namna tunavyochukulia makosa ya watoto wetu. Fikiria namna tunavyowatendea watoto wetu wakikosea.

Fikiria namna tunavyochukulia nidhamu kwa watoto. Fikiria namna tunavyowaamulia watoto badala ya kuwapa fursa kuchagua. Fikiria namna tunavyowawekea watoto mazingira ya kulazimika kutii na kuheshimu kile tunachowaambia.

Fikiria athari za imani ya mzazi kuamini nidhamu ni kusikiliza, kufuata, kutii, kutokosea, tabia ambazo aghalabu humaanisha mtoto kutofikiri, kutokuwa huru kufanya uamuzi wa kujitegemea na kadhalika.

Ukiwachunguza watoto wakiwa wadogo unagundua tunazaliwa na hitaji kubwa la kujifunza. Tangu mapema tunachunguza mazingira yetu, tunapepesa macho kudadisi, tunataka kugusa vitu vinavyotuzunguka, tunasikiliza sauti, mtetemo, tunaonja kinachoonjeka almuradi tukielewe.

Kiu hii ya kuchunguza inakwenda sambamba na kuthubutu na kujaribu. Hatuogopi kugusa, kunusa, kushika, kuonja, kuona kama namna ya kuingia ugunduzi mpya kwenye fahamu zetu.

Katika kujaribu huko panapoleta kujifunza kwingi ndipo penye kukosea. Hatukosei kwa sababu tunataka kuwaudhi wazazi.

Tunakosea kwa sababu tunafanya vingi ambavyo hatujawahi kuvifanya. Tunakosea kwa sababu tunajifunza. Kwa nini sasa tunawaadhibu watoto kwa kukujaribu? Kwa nini tunaadhibu uthubutu wa mtoto kwa kufikiri nidhamu ni kutojaribu mambo mapya? 

Tunapowaadhibu watoto kupindukia tunawajenga kuwa waoga wanaopambana kuturidhisha badala ya kujifunza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *