Rais Pezeshkian: Iran inatafuta haki zake halali katika mazungumzo na MarekaniRais Pezeshkian: Iran inatafuta haki zake halali katika mazungumzo na Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa Iran inatafuta kurejesha haki zake halali katika mazungumzo na Marekani. Hata hivyo, amebainisha kuwa uzoefu mchungu wa majadiliano ya huko nyuma na Washington unaifanya Tehran kusonga mbele kwa tahadhari kubwa na ya kina.

Akizungumza katika kikao na Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Field Marshal Asim Munir, siku ya Jumamosi, Rais Pezeshkian amemshukuru kwa juhudi zake na za serikali yake katika kuimarisha uthabiti na usalama wa kikanda.

Rais Pezeshkian amesema “Watu na viongozi wa Pakistan ni ndugu zetu, na tuna mapenzi ya dhati kwenu. Sisi Waislamu ni mwili mmoja; hatuna budi isipokuwa kuungana. Lazima tujitahidi kupitia ushirikiano kuboresha hali zetu na za Waislamu wote ulimwenguni.”

Rais wa Iran amesisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kutafuta umoja na mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu kupitia suluhu za kivitendo, na kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi, kijamii, kisiasa, na kiutamaduni baina yao.

Akiashiria kujitolea kwa Iran kwa mifumo ya kisheria ya kimataifa, Rais Pezeshkian amesema: “Tunatafuta tu kurejesha haki za taifa letu, lakini historia na uzoefu wetu wa mazungumzo na Wamarekani vinatulazimisha kuwa na tahadhari kubwa.”

Rais wa Iran amesisitiza pia kuwa vita havijawahi kuleta faida kwa yeyote, akiongeza kuwa: “Marekani haitashinda katika mzozo huu. Nchi za eneo hili na dunia nzima ndizo zitakazopata hasara kubwa. Utawala wa Kizayuni ndio upande pekee unaotafuta kulinda maslahi yake katika eneo hili kupitia vita na machafuko.”

Rais Pezeshkian amebainisha kuwa Iran haina imani na Marekani kutokana na ukiukaji wa mara kwa mara wa ahadi zake, mashambulizi wakati wa mazungumzo, na mauaji ya maafisa wa Iran. “Katika mazingira haya, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikitegemea uhusiano wa kindugu na nchi rafiki kama Pakistan, imeanza njia ya mazungumzo,” amesema, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kulinda maslahi ya taifa la Iran kupitia njia zinazofaa.

Kwa upande wake, Field Marshal Asim Munir ameelezea kufurahishwa kwake na mkutano huo na kubainisha kuwa “mchakato wa mazungumzo unaendelea vizuri.” Akimsifu Rais wa Iran, Mkuu huyo wa Jeshi la Pakistan aliongeza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unatafuta maslahi yake kupitia mgawanyiko na mivutano miongoni mwa Waislamu wa eneo.

Kamanda Munir amesisitiza kuwa utawala huo wa Kizayuni una uhasama mkubwa kwa yeyote anayejitahidi kutatua mizozo, na hauna nia ya kuona uthabiti na usalama katika eneo hilo. Amehitimisha kwa kusema kuwa lengo lake ni kurejesha utulivu na kuzuia kuendelea kwa vita, akitarajia kuwa mazungumzo yanayoendelea yatafikia matokeo mazuri kwa Iran na nchi zote za Kiislamu.

Mnamo Februari 28, Marekani na Israel zilianzisha vita haramu dhidi ya Iran kwa kumuua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, raia wa kawaida wakiwemo watoto wa shule, wanasayansi na makamanda kadhaa wa ngazi ya juu wa kijeshi. Katika kujibu uchokozi huo, Majeshi ya Iran yalifanya wimbi 100 la mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya siku 40, yakilenga vituo vya kijeshi vya Marekani na Israel na kusababisha uharibifu mkubwa.

Pakistan ilifanikiwa kupatanisha usitishaji wa vita wa wiki mbili mnamo Aprili 8, jambo lililofungua njia ya mazungumzo. Hatahivyo mazungumzo hayo kati ya Iran na Marekani chini ya upatanishi Pakistan yamekuwa hayajafanikiwa kutokana na  ukaidi wa Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *