UKIACHANA na vita iliyopo ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, imeibuka nyingine ikizihusu Azam na Simba juu ya kuipata saini ya beki wa kulia, Nathaniel Chilambo ambaye mkataba wake ndani ya Azam unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026.
Mabosi wa Simba wanaendelea na mchakato wa kuangalia maeneo ya kuboresha ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, ambapo kwa sasa moja ya eneo linaloangaliwa zaidi ni la beki wa kulia, analocheza Shomari Kapombe.
Kapombe aliyejiunga na Simba Julai 1, 2017, akitokea Azam, amekuwa muhimili mkubwa wa kikosi hicho ambapo kwa sasa mabosi wa timu hiyo wanataka kumtafutia mbadala wake, baada ya kudaiwa kutoridhishwa na kiwango cha David Kameta ‘Duchu’.
Licha ya Duchu kushindwa kuonyesha ushindani zaidi, kwa sasa mabosi wa timu hiyo wanaangalia uwezekano wa kumpata Chilambo ambaye alijiunga na Azam Julai 6, 2022, akitokea Ruvu Shooting.
Inaelezwa kwamba, beki huyo anaweza kuondoka ndani ya Azam mwisho wa msimu huu, pindi mkataba wake utakapoisha, baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Nyota huyo anayemudu pia kucheza beki wa kushoto, amekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kwa sababu ya ushindani uliopo Azam eneo analocheza, huku mshindani wake mkubwa akiwa ni nahodha, Lusajo Mwaikenda.
Licha ya Simba kuonyesha uhitaji wa beki huyo, taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza uongozi wa Azam unadaiwa umemwekea mkataba mpya kwa ajili ya kuendelea naye msimu ujao, jambo linaloongeza ushindani kati ya timu hizo mbili.
Taarifa zinaeleza, Chilambo amefikia makubaliano ya awali na Simba japo hajasaini mkataba rasmi wa kuichezea timu hiyo, huku matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC wakidaiwa wameweka kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuendelea naye.
Hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti, ikiwa Chilambo atasajiliwa atakuwa ni mbadala sahihi wa David Kameta ‘Duchu’ ambaye tangu amesajiliwa Julai 10, 2023, akitokea Mtibwa Sugar, ameshindwa kuonyesha ushindani.
Chanzo hicho kilisema, Chilambo ni mbadala sahihi wa Kapombe tofauti na Duchu, ingawa hata kama nyota huyo atasajiliwa bado uongozi wa Simba unatafuta pia beki mwingine wa kulia wa kigeni atakayeongeza ushindani zaidi msimu ujao kikosini.
