Malaysia: Tutaipeleka Israel ICJ kwa kuteka nyara na kuwatesa wanaharakati wa Freedom FlotillaMalaysia: Tutaipeleka Israel ICJ kwa kuteka nyara na kuwatesa wanaharakati wa Freedom Flotilla

Serikali ya Malaysia iko tayari kuipeleka Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa kosa la kuteka nyara na kuwatesa wanaharakati wa msafara meli za misaada ya kibinadamu wa Global Sumud Flotilla, uliokuwa njiani kuelekea Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Amirudin bin Shari, Waziri Mkuu wa jimbo la Selangor la Malaysia, alisema Jumatatu kwamba Kuala Lumpur itaanzisha kesi mara tu wanasheria watakapokamilisha ukusanyaji wa taarifa na ushahidi unaohitajika.

Zaidi ya wanaharakati 400 wa kimataifa waliokuwa ndani ya meli za msafara huo, ambao ulilenga kuvunja mzingiro wa majini wa Israel dhidi ya watu wa Gaza ili kutoa misaada ya kibinadamu, walishambuliwa na kutekwa nyara na askakri wa Israel wiki iliyopita wakiwa katika maji ya kimataifa.

“Hatutakaa kimya; hatutasita. Wakati timu ya kisheria inakusanya nyaraka zote kuhusu ukiukwaji wa sheria za kimataifa, washiriki katika msafara wa Global Sumud Flotilla walitekwa nyara zaidi ya mara moja, na waliteswa,” amesema Amirudin katika sherehe ya kuwakaribisha nyumbani washiriki wa Global Sumud Flotilla 2.0 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuala Lumpur.

“Tutapeleka suala hili katika mahakama ya kimataifa, tutaendeleza mashinikizo ya kidiplomasia, na pia tutasafiri kote Malaysia,” amesisitiza.

Bin Shari amesema hatua hiyo ya kisheria inafuatia vitendo vya ukatili, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara, mateso na unyanyasaji wa kingono uliofanywa na askari wa Israel dhidi ya wanaharakati wa msafara meli za misaada ya kibinadamu wa Global Sumud Flotilla, hasa washiriki wa Malaysia.

Ameongeza kuwa hatua hiyo itafuatiwa na mashinikizo ya kidiplomasia ya serikali ya kudai “ukombozi kamili” wa Ukanda wa Gaza.

Amesema kwamba Global Sumud 3.0 itaendelea na mapambano dhidi ya utawala wa Israel hadi mzingiro dhidi ya Gaza utakapoondolewa.

Jumatatu iliyopita, askari wa Israel walishambulia kundi hilo katika maji ya kimataifa karibu na pwani ya Cyprus (Kupro).

Shirika la Global Sumud Flotilla limethibitisha kwamba wanaharakati waliotekwa nyara kutoka kwenye meli zilizokuwa zikielekea Gaza walifanyiwa ukatili wa kingono, kushambuliwa kimwili, na kutendewa unyama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *