Dar es Salaam. Maonyesho ya muda ya kuenzi urithi wa mwana diplomasia mashuhuri, Dk Salim Ahmed Salim yaliyozinduliwa wiki hii, yameibua mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa kiuchumi nchini Tanzania, utegemezi wa mitaji ya nje na mustakabali wa ajenda ya maendeleo ya bara la Afrika.
Maonyesho hayo ya mwezi mmoja, yaliyoandaliwa kupitia Salim Ahmed Salim Digital Archives kwa kushirikiana na Jumba la Makumbusho la Taifa, yanaonyesha picha, hotuba, nyaraka za kidiplomasia na mawasiliano ya kihistoria yanayoeleza safari ndefu ya Dk Salim katika diplomasia ya Afrika na ya kimataifa.
Ingawa kumbukumbu za kidijitali za Dk Salim zilishazinduliwa miaka kadhaa iliyopita, waandaaji wanasema maonyesho haya yanalenga kuifanya historia hiyo ipatikane kwa urahisi zaidi kwa wananchi, hususan kizazi kipya kupitia maonesho ya moja kwa moja katika makumbusho.
Akizungumza katika mjadala uliofanyika siku ya ufunguzi, Balozi mstaafu Ami Mpungwe alisema kizazi kilichomwakilisha Dk Salim kilitimiza jukumu lake la kihistoria la ukombozi, umoja wa Afrika na kutambulika kwa bara hilo katika jukwaa la kimataifa.
“Kizazi cha Salim kilitimiza jukumu lake. Sasa swali ni linakuja ni jukumu gani la kizazi hiki cha sasa,” alihoji.
Mpungwe alimsifu Dk Salim kwa kuweka mkazo katika uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu, akisema utamaduni wa kuhifadhi historia bado ni changamoto kubwa barani Afrika.
Alisema maonesho hayo yanatoa fursa muhimu kwa vijana kuelewa si tu matukio ya kihistoria, bali pia fikra na maamuzi yaliyokuwa nyuma ya uamuzi mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia.
Alizungumzia kile alichokiita mkanganyiko wa kiuchumi wa Afrika, ambapo bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali bado linakabiliwa na umaskini wa wananchi wake.
Mkurugenzi wa Diplomasia ya Kiuchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, John Ulanga, alikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa maonyesho ya Dk Salim Ahmed Salim, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU, sasa Umoja wa Afrika – AU), yaliyopangwa na Kengo Limited na kufadhiliwa na Karimjee Foundation katika Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
“Tunawezaje kuwa matajiri na maskini kwa wakati mmoja,” alihoji.
Kwa mujibu wake, nchi nyingi za Afrika zimeanza kuachana na misingi na ahadi zilizokuwa msingi wa harakati za ukombozi, ikiwemo haki ya kijamii, utu na maendeleo jumuishi.
Hiyo ni kwa sababu taasisi za kifedha za kimataifa sasa mara nyingi huweka masharti ya utawala bora, haki za binadamu na huduma za kijamii mambo ambayo Afrika yenyewe iliahidi kuyasimamia wakati wa mapambano ya ukombozi.
“Inafika hatua wale waliotupa uhuru wanatukumbusha ahadi tulizojipa wenyewe,” alisema.
Mpungwe alisisitiza haja ya Afrika kumiliki kikamilifu ajenda zake za maendeleo na mifumo ya kiuchumi badala ya kuendelea kutegemea suluhisho zinazoongozwa kutoka nje.
Mjadala huo pia uliangazia mabadiliko ya jukumu la diplomasia nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Diplomasia ya Kiuchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, John Ulanga alisema diplomasia katika enzi ya Dk Salim ililenga zaidi uungaji mkono wa kisiasa kwa harakati za ukombozi.
Leo, diplomasia imehamia katika kuvutia mitaji, kukuza uwekezaji na kufungua masoko ya kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.
“Jukumu la kizazi hiki ni kukusanya mitaji kutoka duniani kote ili kuikomboa Tanzania na Afrika kiuchumi,” alisema.
Kwa upande wake, Ahmed Salim, mtoto wa mwisho wa Dk Salim alisema maonesho hayo yanaonesha nafasi muhimu ambayo Tanzania imekuwa nayo katika jukwaa la kimataifa.
“Tunachoona kwenye picha ni historia, lakini kilichokuwa kikitokea nyuma ya milango iliyofungwa ndicho kinachofunuliwa kwa mara ya kwanza kupitia maonesho haya,” alisema.
