Damian Soul kama chumvi kwenye msosi wa Hip Hop BongoDamian Soul kama chumvi kwenye msosi wa Hip Hop Bongo

Dar es Salaam. Rapa AY kwenye moja ya mahojiano yake mwaka 2015, aliwataja Damian Soul na Vanessa Mdee kama wasanii wapya anaowakubali sana kutoka kwenye Bongofleva na kuwatabiria makubwa siku za mbeleni.

Damian Soul ambaye alikuja kuvuma na ngoma yake, Mapopo (2020) yenye mahadhi ya Amapiano, hakuna ubishi ni miongoni mwa wasanii wachache Bongo wanaofanya vizuri muziki wa Soul.

Hata hivyo, Damian Soul ameguka kiungo muhimu mfano wa chumvi katika msosi wa Hip Hop Bongo hasa pale linapokuja suala la kuimba kiitikio kitu kilichomfanya kushirikishwa kwenye ngoma kibao za wakali wengi wa muziki huo kama ifuatavyo;

1. Mapito, Kampuni Kubwa – Lord Eyes

Akiwa nje ya kundi la Weusi, mara baada ya kupitia tuhuma mbalimbali kama matumizi ya dawa za kulevya na kuiba vifaa vya gari la Ommy Dimpoz, Lord Eyes aliachia wimbo ‘Mapito’ ambao alimshirikisha Damian Soul kuzungumzia hilo.  

Hakuna ubishi huyu ndiye msanii wa kwanza wa Hip Hop Bongo kugundua sauti ya Damian Soul inauzika kwa urahisi zaidi kwenye muziki huo hasa akisimama upande wa kiitikio, na Januari 2021 akimshirikisha tena Damian katika ngoma yake, Kampuni Kubwa.

2. My Power -Young Killer

Baada ya kuachia ngoma yake, Dear Gambe aliyofanya na Belle 9 ambayo ilimtambulisha kwenye muziki hadi kushinda tuzo za TMA 2014, kisha ‘Miss Super Star’ akiwa na Bright na Nemo, ikiwa ni zamu ya Damian Soul.

Kwa ujumla Young Killer alikuwa na utaraibu kufanya kazi wasanii wanaojua kucheza na sauti zao vizuri, hivyo basi akampa shavu Damian Soul katika wimbo wake ‘My Power’ uliofanya vizuri.

3. Mistari Yako – ZaiiD

Aliyekuja kujizolea umaarufu mkubwa na ngoma yake ‘Wowowo’, ZaiiD pia ni mzuri kufanya cover za nyimbo za wasanii wa nje kwa lugha ya Kiswahili, alishafanya hivyo katika ngoma ya J Cole ‘Who Dat’ na ile ya FettyWap ‘Trap Queen’ ila akiipa jina la Madebe.    

ZaiiD alimshirikisha Damian Soul kwenye ngoma yake ‘Mistari Yako’ ambayo anazungumzia kuumizwa kimahusiano baada ya kushindwa kunufaika na muziki wake licha ya kutia juhudi kubwa kwa muda mrefu.

4. Kila Sababu – Mansu-Li

Alipendelea kujiita Sinza Star, ni Rapa aliyedumu kwa muda sasa kwenye Bongofleva tangu atoke na ngoma yake, Kina Kirefu. Mansu-Li mwaka 2013 aliachia albamu inayokwenda kwa jina hilo.

Mansu-Li naye alitambua uwezo wa Damian Soul upande wa kulainisha ngoma ngumu na kuamua kufanya naye kazi, wakaingia studio za Tongwe Recods na kuachia ngoma, Kila Sababu.

5. I Know You Now – Songa

Alitoka kimuziki chini ya mikono ya Duke Tochez baada ya kusainiwa M Lab (Music Laboratory) na sasa anawika katika kundi la Kikosi Kazi, Songa naye hakuwa mbali kuinasa sauti ya Damian Soul.

Songa alimshirikisha Damian Soul katika wimbo ‘I Know You Now’ ulioachiwa mtandaoni tu ambapo ana mauzo makubwa, amewahi kushinda tuzo zinazotolewa na tovuti ya kuuza muziki, Mdundo.com kama Msanii Bora ya Hip Hop baada ya kufikisha ‘downloads’ zaidi ya 300,000.

6. Yeye – One The Incredible

Mkali huyu wa midondoko katika Hip Hop kutokea Tamaduni Muzik na kundi la Kikosi Kazi ni mara chache kuwashirikisha waimbaji katika ngoma zake, miongoni mwa wachache waliopata bahati hiyo ni Damian Soul.

One The Incredible alimshirikisha Damian Soul kwenye wimbo wake ‘Yeye’ uliyotayarishwa studio za Mandugu Digital, wimbo huu unapatikana kwenye albamu yake ya pili, RAP (Representing Africa Popote) iliyotoka Desemba 2014.

7. Masihara – Motra The Future

Ni Rapa ambaye lafudhi yake katika Hip Hop inatambulisha kule anapotokea, Motra The Future baada ya kolabo na wakali kama Ruby na G Nako alimshirikisha Damian Soul katika wimbo wake, Masihara.

Wimbo huo ambao alishirikishwa na Shetta, baadaye ulikuja kufanyiwa remix ambapo mshindi wa Big Brother Africa Hotshots 2014, Idris Sultan alipewa nafasi ya kusikika ukiwa ni wimbo wake wa kwanza tangu kuwa maarufu.

8. Too Much – Joh Makini

Rapa huyu kutoka kundi la River Camp Soldiers na sasa Weusi alimpa shavu Damian Soul katika ngoma yake ‘Too Much’ ikiwa ni ngoma ya tatu kufanya pamoja kwa ujumla.

Damian amemshirikisha Joh Makini kwenye nyimbo zake mbili; Ni Penzi na Baraka ambazo kwa nyakati tofauti zilifanya vizuri, wimbo ‘Ni Penzi’  ulichaguliwa kuwania tuzo za TMA 2014 katika kipengele cha Wimbo Bora wa R&B lakini kwa bahati mbaya haukuweza kushinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *