Dar es Salaam. Msanii wa vichekesho nchini, Anko Nzala amesema ukaribu wake na mfanyabiashara mkubwa Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ulianza kitambo kupitia biashara zake na mapenzi yao kwa klabu ya Simba SC.
Anko Nzala wakati akizunguza na Mwananchi amesema mahusiano yao hayakuanza ghafla kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodhani. Bali yalijengwa kwa muda mrefu kutokana na kufuatilia bidhaa mbalimbali za mfanyabiashara huyo pamoja na ushabiki wa soka.
Akizungumzia video yao iliyosambaa kwa kasi mitandaoni, mchekeshaji huyo amesema wazo la kuandaa maudhui hayo lilizaliwa baada ya mazungumzo yaliyohusu biashara za Mo. Hali iliyompa wazo la kuingiza utani wa wapinzani wa kibiashara kwenye kazi hiyo.
“Niliona kwa nini nisiingize biashara za wapinzani wake kwenye content ili iwe na ladha tofauti kidogo,” amesema Anko Nzala.
Amesema baada ya kumpa Mo wazo hilo, alilipokea vizuri na kukubali kushiriki bila kusita jambo lililofanikisha kurekodiwa kwa video hiyo iliyozua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, Anko Nzala amesema bado kuna baadhi ya watu hawaamini kama kweli aliweza kufanya kazi na Mo Dewji. Huku wengine wakidai video hiyo ilitengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI).
Kwa mujibu wa Anko Nzala, madai hayo hayawezi kumbadilisha, kwani anafahamu watu wengi walishangazwa na ukaribu wao kiasi cha kuona kama jambo hilo haliwezekani.
“Wapo wanaosema ile ni AI lakini ukweli ni kwamba tulikutana na kufanya kazi ile kama kawaida,” amesema.
Mchekeshaji huyo amesema tangu content hiyo isambae, imeongeza kiwango cha imani kutoka kwa mashabiki wake. Huku watu wengi zaidi wakianza kufuatilia kazi zake na kuzitambua.
Amesema mafanikio hayo yamempa hamasa ya kuendelea kuboresha maudhui yake ili yaweze kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumzia mabadiliko yake kutoka komedi ya kuongea hadi ya kimya (silent comedy) Anko Nzala amesema alifikia uamuzi huo baada ya kutamani kuifikisha komedi ya Tanzania kimataifa bila kuzuiwa na lugha.
Amesema hapo awali alijaribu kufanya komedi kwa lugha ya Kiingereza lakini aligundua uwezo wake wa lugha hiyo haukuwa mzuri, kiasi cha kuweza kufikisha ujumbe alioutaka kwa ufanisi.
Kutokana na hali hiyo, amesema akaona njia bora ni kufanya komedi ya kimya kimya ambayo mtu yeyote anaweza kuelewa bila kujali taifa au lugha anayotumia.
Pamoja na mafanikio ya content yake na Mo Dewji, Anko Nzala amesema hakupata changamoto yoyote wakati wa kurekodi video hiyo. Amesema walifanikiwa kupiga “take one” kutokana na Mo kuelewa haraka maudhui yote yaliyokuwa yanahitajika.
Aidha, amewatoa hofu mashabiki wake kwa kusema bado ana mipango mingi mikubwa ijayo huku akidokeza uwezekano wa kufanya tena kazi nyingine na Mo Dewji siku zijazo.
