KUNA asilimia kubwa za kiungo mshambuliaji wa Yanga, Celestin Ecua msimu ujao akatolewa tena kwa mkopo au kuvunjiwa mkataba wake na klabu hiyo, huku taarifa zikibainisha kwamba, hata huko alipo sasa hali si nzuri.
Dirisha dogo la Januari 2026, nyota huyo raia wa Chad alitolewa na Yanga kwa mkopo kwenda JS Kablylie ya Algeria.
Ecua aliyewahi kung’ara akiwa na Zoman FC msimu uliopita na kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, alisajiliwa Yanga kwa matumaini makubwa ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji, lakini mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa.
Nyota huyo alikuwa akipata nafasi ya kuanza kikosini chini ya aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Pedro Goncalves lakini ilionekana alishindwa kuendana na falsafa ya klabu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Yanga iliamua kumpeleka kwa mkopo JS Kabylie kwa lengo la kumpa nafasi ya kurejesha kiwango chake.
Makubaliano ya mkopo huo yalikuwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja endapo angeonyesha kiwango cha kuridhisha.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hata huko Algeria mambo hayajawa mazuri kwa mchezaji huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto.
Takwimu zinaonyesha Ecua amekuwa akipata nafasi ndogo ya kucheza, mechi nyingi akiishia benchi au kutokuwa kabisa kwenye kikosi.
Ni mechi tatu kati ya kumi alizocheza nyota huyo ndiyo ameanza. Katika mechi dhidi ya Paradou alicheza dakika 90, huku akicheza dakika 46 dhidi ya JS Saoura na Khenchela ambapo hakufunga zaidi ya kutoa asisti moja. Jumla ametumika kwa dakika 283.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, JS Kabylie haipo tayari kumnunua nyota huyo kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake.
Hata hivyo, inaelezwa Yanga pia haina mpango wa kuendelea na huduma ya mchezaji huyo, huku ikimweleza aanze kutafuta timu nyingine.
“Tunaangalia kama tutaweza kumvunjia mkataba, tulimtoa kumuangalia labda hakuzoea hali ya Tanzania na kule Algeria pia imekuwa changamoto kwake, kwa hiyo tutakaa vizuri tujue tunafanyaje kati ya machaguo hayo mawili,” kilisema chanzo cha ndani.
Nyota huyo katika kipindi cha takribani miezi sita akiwa Yanga, alicheza mechi nane na kufunga bao moja.
Mbali na Ecua, nyota wengine ambao Yanga iliwatoa kwa mkopo ni Balla Moussa Conté kwenda Raja Casablanca ambapo amecheza mechi mbili, huku Mohamed Doumbia akipelekwa Marumo Galants ya Afrika Kusini akifanikiwa kucheza mechi kumi nchini humo akifunga mabao mawili.
Hivi karibuni, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema wanawafuatilia wachezaji waliowatoa kwa mkopo kujua maendeleo yao, kisha benchi la ufundi litaamua hatma ya kuendelea nao au la pindi ripoti ikifika mezani.
