Nyota Fountain Gate ataja yanayowabeba Ligi KuuNyota Fountain Gate ataja yanayowabeba Ligi Kuu

WAKATI mashabiki na wadau wa soka nchini wakishangaa na matokeo waliyonayo hivi sasa Fountain Gate na kiwango bora cha wachezaji, kiungo wa timu hiyo, Ismail Aziz Kader ameeleza sababu za kung’ara kwao, huku akitaja mambo mawili nyuma yao.

Fountain Gate haikuwa na mwanzo mzuri Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kwa sasa wameonekana kuamka tangu benchi la ufundi kuwa chini ya Kocha Mkuu, Fredi Felix ‘Minziro’ na msaidizi wake Wandiba Mathias.

Minziro aliikuta timu hiyo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 16 ambapo tayari ameiongoza michezo tisa akishinda minne, sare moja na kupoteza mitatu, kikosi hicho kikipanda hadi nafasi ya tisa kwa pointi 29.

MINZI 01

Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo mwenye mabao matano na asisti nne, amesema ujio wa Minziro na muunganiko wa nyota kikosini haswa eneo la ushambuliaji ndio siri kubwa ya mafanikio kwa sasa.

Amesema kombinesheni ya nyota wenzake, Henry David mwenye mabao matatu na Juma Abushir aliyefunga mabao mawili na asisti moja, imeongeza nguvu kubwa kikosini kwani wamekuwa na maelewano mazuri nje na ndani ya uwanja.

“Kwanza Kocha ametuongezea vitu vingi haswa hamasa uwanjani, ameituliza timu ukizingatia hatukuwa na mwanzo mzuri, lakini tumekuwa na uelewano mzuri katika eneo la mbele.

“Kila mchezaji amekuwa na wajibu na jukumu la kuipambania timu na tumekubaliana tusirudie yaliyotukuta msimu uliopita, binafsi kama mchezaji mzoefu wa ligi, nimekuwa na ukaribu sana na Abushir na tunasikilizana,” amesema nyota huyo.

MINZI 02

Amesema kutokana na mwenendo mzuri walionao kwa sasa, wanahitaji kuendelea kupambana kwani pointi walizonazo si salama sana.

Wakati Minziro anatua Fountain Gate Aprili 11, 2026, siku tatu nyuma klabu hiyo ilipigwa tafu na PigaBet ikipewa udhamini wa Sh1 bilioni kwa mkataba wa miaka minne ambao lengo ni kuongeza ushindani, kuhamasisha wachezaji, kukuza ushiriki wa mashabiki na kuchangia maendeleo ya soka la Tanzania.

Udhamini huo ulikuja wakati Fountain Gate ikiwa kwenye presha kubwa ambapo timu hiyo ilikuwa karibu na eneo la hatari baada ya kupitia kipindi kigumu cha matokeo yasiyoridhisha, changamoto za uwanjani na hofu ya kushuka daraja.

Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau, amesema sehemu ya udhamini huo imehusisha motisha kwa wachezaji kulingana na matokeo ya ligi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *