
Dar es Salaam. Katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara zinazotarajiwa kuchezwa kumaliza mzunguko wa 25, Singida Black Stars pekee ndiyo ina nafasi ya kubadilisha nafasi kutoka sasa iliyopo endapo ikishinda, lakini zingine hata zikishinda, zitaendelea kubaki palepale kwenye msimamo, zaidi kuongeza pointi.
Mechi hizo mbili za kumaliza mzunguko wa 25 zinapigwa leo Jumanne ambapo mapema saa 8:00 mchana, Pamba Jiji itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons, wakati saa 10:15 jioni, Singida Black Stars inaikaribisha Mbeya City.
Jiji la Mbeya leo litakuwa kwenye maombi makubwa yatakayoelezwa kwa timu zao ambazo hazipo katika nafasi nzuri ukiangalia msimamo wa ligi. Tanzania Prisons ni ya 15, wakati Mbeya City inakamata nafasi ya 14. Zimepishana pointi tano.
PAMBA JIJI VS PRISONS
Kutokana na orodha ya wafungaji wa timu ya Pamba Jiji sambamba na wale wa Tanzania Prisons ambapo timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, inaonesha haitakuwa yenye mabao mengi.
Pamba Jiji iliyopo nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ikicheza mechi 24, imeshinda nane, sare tisa na kupoteza saba ikivuna pointi 33, ikifunga mabao 23, kinara wake akiwa Mathew Tegisi aliyefunga matano, anafuatiwa na Peter Lwasa (3). Timu hiyo ikishinda itafikisha pointi 36 ikiendelea kusalia nafasi ya saba nyuma ya TRA United yenye 37.
Mbali na mabao 23 yanayomilikiwa na timu hiyo, imetikiswa nyavuni zake mara 24, huku kipa Yona Amosi akiwa na cleansheets saba, amebakiza nne kufikisha 11 alizomaliza nazo msimu uliyopita.
Kwa Prisons iliyopo nafasi ya pili kutoka mwisho (15) katika mechi 24 imeshinda nne, sare tano, imepoteza 15 na kumiliki pointi 17, hata ikishinda dhidi ya Pamba Jiji itafikisha alama 20, ikiendelea kusalia hapo ilipo.
Jumla ya mabao 12 ya timu hiyo, George Mpole ndiye kinara wao akifunga matano na beki Oscar Mwajanga aliye na mawili wamechangia zaidi ya nusu, lakini pia ukuta wao unaruhusu sana mabao kwani wametikiswa mara 34, huku golikipa Mussa Mbisa akiwa na Cleansheets sita, akizidi moja ya msimu uliyopita alipokuwa na tano.
Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema: “Japokuwa tukishinda mechi tutasalia nafasi ya saba lakini tutakuwa tumefikisha pointi 36, kwani TRA United iliyo nafasi ya sita ina pointi 37 lakini ni vizuri tukaendelea kuongeza alama ili huku mbele itatusaidia kupanda nafasi za juu.”
Kwa upande wa kocha wa Prisons, Shadrack Nsajigwa amesema: “Hatuna namna nyingine zaidi ya kushinda mechi hii kwani tupo nafasi mbaya, tunahitaji kujiondoa katika presha, tukishinda tutaongeza pointi ila tutasalia nafasi ileile lakini inaweza ikatusaidia kwa baadaye kupanda juu kwenye msimamo wa ligi.”
SINGIDA BS VS MBEYA CITY
Singida iliyopo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikicheza mechi 24, imeshinda 11, sare tano, imepoteza nane, ina pointi 38 ikifunga mabao 30, kinara wake wa ufungaji ni Mossi Ndumumwe (mabao manane), nyavu zao zimetikiswa mara 26 huku golikipa mwenye cleansheets nyingi ni Amasa Obasogie (5), jambo linaloonyesha ukuta unaruhusu mabao mengi.
Singida kwa sasa ina pointi sawa na JKT Tanzania, lakini zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa yanayoiweka Singida nafasi ya tano, kwenye msimamo, hivyo ikishinda au sare, itarejea kukaa nne bora.
Kwa Mbeya City iliyopo nafasi ya 14, katika mechi 24 imeshinda tano, sare saba na imepoteza 12, ikuvuna pointi 22, katika jumla ya mabao 19 inayomiliki kinara ni Eliud Ambokile (4) akifuatiwa na Vitalis Mayanga (3), lakini pia ukuta wao ni namba mbili kwa kuruhusu mabao mengi ambayo ni 35 ukiacha kinara KMC iliyotikiswa nyavuni mara 40. Golikipa wa Mbeya City, Beno Kakolanya ana cleanstees tatu.
Mbeya City ina pointi 22, ikishinda itafikisha 25 ilizonazo Namungo iliyokuwa uwanjani jana kucheza dhidi ya Yanga, hata hivyo, Mbeya City imeachwa kwa tofauti ya mabao, hivyo ushindi kwake utaifanya kusalia nafasi ya 14.
Mshambuliaji wa Mbeya City, Ambokile amesema: “Tuna kazi kubwa ya kufanya ili kujiondoa katika presha ya kushuka na kucheza mtoano, kila mechi kwetu tunaichukulia kama fainali.”
Wakati huo huo, kocha wa Singida BS, Muhibu Kanu amesema: “Tumetoka kufungwa na Yanga kwa mabao 3-0, mechi inayokuja kwetu tunahitaji ushindi, ingawa tunafahamu Mbeya City ipo nafasi mbaya, lakini kila timu inapambania malengo yake.”
