Viongozi wamlilia mama wa MagufuliViongozi wamlilia mama wa Magufuli

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa Serikali wametuma salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli kufuatia kifo cha mama yake mzazi, Suzana Magufuli.

Suzana alifariki dunia nyumbani kwake Chato, Mkoa wa Geita saa 1 jioni ya jana Jumatatu, Mei 25, 2026 baada ya kuugua kwa muda mrefu huku taarifa za msiba huo zikithibitishwa na mjukuu wake, Jesca Magufuli ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita.

“Bibi yetu amefariki saa moja usiku nyumbani kwake Chato baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taratibu za msiba familia itawajulisha. Bwana ametoa na Bwana ametwaa,” amesema Jesca akizungumza na Ayo TV.

Mama wa Magufuli, anafariki dunia ikiwa ni siku 1895 tangu alipomzika mwanaye John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Kufuatia msiba huo, Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za rambirambi akisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho na kuungana na familia ya Hayati Magufuli katika kipindi hicho kigumu.

Katika salamu zake, Rais Samia amesema kifo hicho kimeligusa taifa kutokana na nafasi ya familia ya Hayati Magufuli katika historia ya nchi.

“Kwa niaba ya Serikali na kwa niaba yangu binafsi, naungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, tukiwaombea nguvu, faraja na uvumilivu,” amesema Rais Samia kupitia taarifa kwa vyombo vya Habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bakari Machumu.

Alimuombea marehemu apumzike kwa amani huku akiwasihi Watanzania kuendelea kuiombea familia hiyo.

Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi naye ni miongoni mwa waliotuma salamu za rambirambi akisema anaungana na Rais Samia pamoja na Watanzania wote katika kuifariji familia ya Hayati Magufuli.

“Ninaungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan, katika kutoa pole na kuwafariji familia na waombolezaji wote kufuatia kifo cha Bi Suzana Magufuli,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema anamwombea marehemu apate pumziko la milele huku familia ikipewa subira na nguvu katika kipindi hicho cha maombolezo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo hicho akieleza kuwa msiba huo si wa familia pekee bali ni wa Watanzania wengi walioguswa na mchango wa familia ya Hayati Magufuli kwa taifa.

“Msiba huo sio wa familia pekee bali ni wa Watanzania wote walioguswa na mchango mkubwa wa familia hiyo kwa taifa,” amesema Dk Mwinyi katika salamu zake za pole.

Ameifariji familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu huku akiwaomba wawe na subira, mshikamano na uvumilivu katika kipindi hicho kigumu.

Hayati Suzana Magufuli alikuwa akifahamika kama mlezi na nguzo muhimu ya familia ya Hayati Magufuli, aliyeiongoza Tanzania kuanzia Novemba 5, 2015 hadi Machi 17, 2021, alipofariki dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *