
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, amesema nchi yake inaunga mkono msukumo wa Afrika wa kutaka fidia kutoka kwa madola ya kikoloni. Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Afrika mjini Moscow, Lavrov amesema suala hilo ni sehemu ya mapambano mapana dhidi ya ukoloni mambo-leo.
Akihutubia wanadiplomasia na maafisa wa Afrika mjini Moscow, Lavrov amesema mataifa ya zamani ya kikoloni yanaendelea kunufaika na utajiri mkubwa wa maliasili za Afrika huku nchi nyingi za bara hilo zikiendelea kutegemea mifumo ya kifedha na viwanda inayodhibitiwa kutoka nje.
Ameusifu Umoja wa Afrika kwa kuendeleza kaulimbiu yake ya mwaka 2025 inayolenga “haki kwa Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika kupitia fidia.” Kwa mujibu wa Lavrov, Moscow inaitazama kampeni hiyo kama juhudi za kurejesha “haki ya kihistoria” na kufuta athari za utawala wa kikoloni.
Lavrov pia ameashiria azimio jipya la Umoja wa Mataifa lililotambua biashara ya utumwa ya kuvuka Atlantiki kuwa “uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya ubinadamu.” Azimio hilo lilipata uungwaji mkono wa mataifa 123, yakiwemo Russia na China, huku Marekani, utawala wa Israel na Argentina zikilipinga. Mataifa 52, yakiwemo Uingereza na wanachama wa Umoja wa Ulaya, yalijizuia kupiga kura.
Lavrov amesema “Russia inaunga mkono kikamilifu mwamko wa pili wa Afrika, na utambuzi wa Waafrika kuhusu haja ya dharura ya kujikomboa mara moja kutoka kwa minyororo ya ukoloni mambo-leo katika sura zake za kisasa.”
Waziri huyo wa Russia pia amezungumzia kuongezeka kwa ushirikiano wa biashara, usalama, elimu na diplomasia kati ya Russia na mataifa ya Afrika.
Lavrov pia alithibitisha kuwa Russia itaandaa Mkutano wa Tatu wa Russia na Afrika mwezi Oktoba, akisema Kremlin inatarajia viongozi wa Afrika kuidhinisha ramani mpya ya ushirikiano wa miaka mitatu ijayo.
