
Guterres amesema hayo kwenye Kongamano la Kimataifa la 2026 la Kupunguza Umaskini na Kuchochea Maendeleo duniani lililofanyika nchini China, ambapo hotuba yake imesomwa kwa niaba yake na Mratibu Mkazi wa UN nchini humo, Stephen Jackson.
Vichocheo vya umaskini duniani
Pamoja na kushukuru China kwa kuandaa kongamano hilo la siku moja, Katibu Mkuu amesema kuwa umaskini bado ni “dharura ya kimataifa ya maendeleo,” akibainisha kuwa takriban watu milioni 800 bado wanaishi katika umaskini wa kupindukia katika maeneo ya vijijini na mijini duniani kote.
Amesema migogoro, mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na madeni makubwa vinaendelea kuzidisha hali kwa jamii zilizo hatarini.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza matumaini kwamba ushirikiano wa kimataifa na majadiliano katika kongamano hilo vinaweza kusaidia kupata suluhisho za vitendo.
Wito wa kuongeza uwekezaji
Katibu Mkuu huyo amezihimiza serikali kuongeza uwekezaji katika ajira zenye staha, elimu, huduma za afya, maendeleo endelevu ya vijijini na mifumo ya ulinzi wa kijamii kwa wote.
Pia amesisitiza kuwa nchi zinazoendelea zinahitaji ufadhili mkubwa zaidi na nafasi pana ya kifedha ili kusaidia malengo ya maendeleo ya muda mrefu.
Mageuzi ya mfumo wa kifedha wa kimataifa
Guterres amerejelea Ahadi ya Sevilla iliyopitishwa mwaka jana, ambayo inataka hatua za haraka za kuongeza ufadhili wa maendeleo, kupunguza mzigo wa madeni kwa nchi maskini na kufanya mageuzi katika mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao aliuelezea kuwa usio wa haki.
Pia ametaja Mkutano wa Maendeleo ya Kijamii duniani, uliotoa wito wa sera madhubuti zaidi za kijamii na uwekezaji unaolenga kupunguza umaskini, ukosefu wa usawa na kutengwa kwa jamii.
Watu ndio kipaumbele
Akihitimisha ujumbe wake, Guterres amesema jamii ya kimataifa lazima ifanye kazi pamoja kujenga uchumi unaoweka “watu mbele” na kuendeleza mapambano ya kimataifa ya kupunguza na hatimaye kutokomeza umaskini.
