Suala la maridhiano ya kitaifa limekuwa likipigiwa chapuo na watu wa makundi tofauti, wakihitaji maridhiano ya dhati yenye lengo la kuliponya taifa kutokana na makovu yaliyosababishwa na mauaji baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wengine wanaenda mbali zaidi wakisema maridhiano yalihitajika hata kabla ya Oktoba 29 kwani taifa halikuwa moja, matukio ya utekaji na mauaji yalichochea hofu na watu kukamatwa katika utaratibu unaopingwa.
Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ezekia Wenje ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba maridhiano yanahitajika haraka kwani yamechelewa mno huku akimtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuitisha maridhiano hayo haraka.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Wenje nyumbani kwake Kigamboni, Dar es Salaam ambapo ameangazia masuala tofauti ya kisiasa na kijamii ikiwemo umoja wa kitaifa, maridhiano na Katiba mpya.
Mkwamo wa Katiba mpya
Wenje ambaye alikuwa Mbunge wa Nyamagana kupitia Chadema kabla hajatimkia CCM, anasema wajumbe wa upinzani waliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushindwa kukubaliana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014 na kususa, akiwamo yeye, walifanya kosa ambalo limechangia nchi kuendelea kuwa na migogoro ya kisiasa hadi leo.
Anasema hiyo ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na mapenzi ya kweli kwa taifa, akieleza uzoefu wake ndani ya Chadema na namna mazungumzo ya kisiasa yalivyowahi kuleta mafanikio na jinsi kutokubaliana kulivyoathiri safari ya mageuzi nchini.
Mwanasiasa huyo aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, anasema alishiriki kwa miaka mingi katika vikao vya juu vya Chadema, hivyo anafahamu kwa undani historia ya mazungumzo ya kisiasa kati ya upinzani na Serikali.
Anasema wakati wa mjadala wa Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, kundi la Ukawa lilisusia Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu ya msimamo wa kutaka mfumo wa serikali tatu huku upande mwingine ukisisitiza mfumo uliopo sasa wa serikali mbili.
“Niliwambia tusifike huko, ni kama mfano mtu unamdai Sh100,000, akakuletea Sh50,000 au hata Sh40,000, akakwambia chukua hii, iliyobaki nitakulipa, halafu unaikataa hata hiyo nusu, ndicho kilitokea wakati ule.
“Ishu ilikuwa ni moja tu, sisi (Ukawa) tulitaka Serikali tatu, wenzetu walitaka mbili, tukasusa, hali ile imefanya nafasi muhimu ya kupata baadhi ya mabadiliko ambayo yangesaidia kupunguza migogoro ya kisiasa.
Anasema rasimu ya Jaji Warioba ilikuwa ina ‘offer’ ya mambo mengi mazuri ikiwamo hata muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vitu vingine vingi, lakini wao (Ukawa) waliondoka kwa sababu walitaka serikali tatu na upande mwingine uling’ang’ana na serikali mbili.
“Tukiwa pale bungeni niliwambia wenzangu there is no way (hakuna njia), tukubaliane kwa kuwa katiba ya nchi sio Bibilia wala msaafu kwamba ikishakuwa haiwezi kubadilika, tukubaliane na haya.
“Tungebaki pale, tukachukua yale tuliyokubaliana halafu tukaendelea kudai mengine, huenda leo tusingekuwa hapa.
“Negotiation (majadiliano) yoyote duniani huwezi kupata kila kitu unachotaka, tatizo letu kubwa lilikuwa kutokubaliana mwaka 2014 kwenye Bunge Maalumu la Katiba,” anasema Wenje.
Maridhiano siyo uoga
Wenje anasema yaliyotokea Oktoba 29 yanasikitisha na hayakuwahi kuwa sehemu ya utamaduni wa siasa za Tanzania, akirejea ripoti ya Tume ya Jaji Mohamed Chande iliyoeleza kwamba watu 518 walifariki dunia pamoja na hasara za kiuchumi zilizotokana na vurugu hizo.
Anasema sekta binafsi ilipoteza mabilioni ya fedha huku biashara mbalimbali zikiharibiwa, vikiwamo vituo vya mafuta na viwanda vilivyoajiri vijana wengi.
Anatoa mfano wa mwanamke aliyekutana naye Mwanza ambaye alipoteza ajira baada ya kiwanda alichokuwa akifanya kazi kuchomwa moto wakati wa vurugu hizo.
Pamoja na maumivu hayo, Wenje anasema suluhisho la kudumu haliwezi kupatikana bila mazungumzo ya kisiasa.
Anatolea mfano matukio ya kimataifa yakiwamo mazungumzo kati ya Israel na Palestina pamoja na mvutano wa kisiasa nchini Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, akimtaja aliyekuwa mwanasiasa nguli wa upinzani Raila Odinga (sasa marehemu) kama mfano.
“Licha ya Odinga kuamini aliibiwa ushindi mara kadhaa, bado alikubali kukaa mezani na wapinzani wake akiwamo Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na William Ruto kwa mihula tofauti yote ikiwa ni kwa ajili ya kuokoa nchi yao,” anasema.
Vilevile, anasema akiwa Chadema walikwenda kwenye mazungumzo ya maridhiano na Chama cha Mapinduzi (CCM), wakapeleka hoja mezani ikiwamo kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa, kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara, kurejea kwa wakimbizi wa kisiasa na madai ya Katiba mpya.
“Baadhi ya mafanikio yalipatikana kupitia mazungumzo hayo, ikiwamo kuondolewa kwa wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi, jambo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likilalamikiwa na vyama vya upinzani.
“Changamoto kubwa huwa ni upande mmoja kutaka kupata kila kitu kwa asilimia 100, niseme hili tu kwa uwazi, kwamba anayekubali kwenda kwenye maridhiano si mwoga wala msaliti, bali ni mtu mwenye uwezo wa kuweka maumivu yake pembeni kwa ajili ya maslahi ya taifa.
“Kwenda kwenye mazungumzo siyo uoga, siyo kusurrender, ni ukomavu na kuonyesha jinsi gani mnavyoipenda nchi yenu, kwamba pamoja na maumivu tunayopitia bado tuko tayari kuzungumza kwa ajili ya mama Tanzania,” anasema Wenje.
Anasema mazungumzo ya maridhiano yanachelewa, hivyo anamtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuwaita walio tayari ili mazungumzo yaanze, na hao wengine ambao hawako tayari watakuja mazungumzo yakiwa yameshaanza.
“Nchi hii ni kubwa kuliko mtu, kuliko chama chochote cha siasa, kwa hiyo, for the sake of our country (kwa ajili ya nchi yetu), mazungumzo yaanze. Ninachomwambia Rais ni kwamba anachelewa, mazungumzo ya maridhiano yaanze,” anasema Wenje.
Wenje anaeleza hayo zikiwa zimepita wiki chache tangu makamu mwenyekiti wa Chadema, John Heche, katika mahojiano na Mwananchi, alipotoa masharti mawili kwa Rais Samia Suluhu Hassan akieleza kwamba chama hicho kitafikiria kwenda kwenye maridhiano endapo mwenyekiti wao, Tundu Lissu aliyeko mahabusu ataachiwa huru na chama kuruhusiwa kuendelea na shughuli za kisiasa.
Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini inayoendelea Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam huku chama hicho kikiwa tayari kimeondolewa zuio la kimahakama la kutofanya shughuli za kisiasa kufuatia wanachama wake upande wa Zanzibar kufungua kesi ya mgawanyo wa rasilimali.
Hali ya kisiasa nchini
Wenje anagusia hali ya kisiasa kwa sasa nchini na kueleza sio mbaya, japo taifa limepitia kipindi kigumu baada ya vurugu zilitokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana.
“Yalitokea mambo mengi lakini toka mwaka jana mpaka sasa kuna utulivu kwa kiasi kikubwa sana katika nchi yetu, nasema hali ya kisiasa ni nzuri kwa sababu shughuli za kisiasa zinaendelea, vyama vya siasa vinafanya kazi zao za kisiasa.
“Tunaona Chadema wako kwenye mikutano yao maeneo mbalimbali, kwa hiyo ni ukweli kwamba kuna stability kwa maana kuna utulivu shughuli za kisiasa zinaendelea na hata shughuli za kijamii zinaenda kama kawaida, kwa hiyo hali ya kisiasa Tanzania kwa sasa inaridhisha,” anasema.
Alijifunza siasa kwa Odinga
Wenje ambaye alitoka kwenye kuajiriwa, akiwa mtumishi wa benki na kuingia kwenye siasa, anaeleza namna Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, kati ya mwaka 2008 – 2013, alivyokuwa mfano wa kuigwa kwake katika siasa.
Anasema alibahatika kuwa karibu na mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Kenya na kushiriki naye katika mambo mbalimbali.
“Nimesafiri naye nje ya nchi, wakati mwingine nambeba na mkoba wake, alikuwa ni mtu ambaye niko naye karibu sana, nikienda Nairobi mara nyingi niko naye, akija hapa Tanzania tunaonana, alikuwa kiongozi wa kuigwa katika siasa.
“Ukiangalia uchaguzi ulioleta shida kubwa sana Kenya ni uchaguzi wa mwaka 2007, chama cha kina Raila kiliamini waliibiwa kura, watu wake wakawa wanasema ikiwezekana wajitenge hata Kenya, kuanzia Eldoret kwenda mpaka Kisumu wajitenge wawe ni nchi yao binafsi,” anasema.
Anasema katika hilo, bado Raila alikataa kwa sababu anaipenda nchi yake, huyo ndiye amekuwa mfano wa kuigwa katika siasa zake.
Akieleza namna alivyokuwa karibu na kiongozi huyo, Wenje anasema msaidizi binafsi wa Raila ambaye alikuja kuwa mbunge baadaye nchini Kenya, alikuwa na undugu naye, hivyo alipenda siasa za Odinga na kuwa mfano wake wa kuigwa.
“Unafahamu sisi wajaluo kila sehemu tupo, unaweza kukuta shangazi yangu aliolewa Kenya, hivyo yule msaidizi wa Raila akawa ni binamu yangu, mara kadhaa nimekuwa nikimtembelea baba (Raila) Kenya na hata nilipokuwa na matukio yangu nikiwa mbunge aliwatuma watu kuja kuungana nami,” anasema.
